WAZIRI JAFFO ATOA MAELEKEZO KARIAKOO

 

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Suleiman Jaffo ametoa wiki mbili kwa maofisa biashara wa mkoa wa Dar es Salaam kutoa taarifa ya wageni kutoka nje ya Tanzania wanaofanya biashara ya uchuuzi, ambayo ingeweza kufanywa na Watanzania.

Waziri Jaffo amesema hayo leo Dar es Salaam wakati akijitambulisha kwa viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania na kuahidi kushirikiana nao, ili kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara nchini kwa ujumla.

Akizungumzia wachuuzi amesema ataanza na Jiji la Dares Salaam ili kupatikana kwa orodha yao na hakutakuwa na aibu kuwafuatilia.

Amesema wawekezaji wanaokuja nchini wanatakiwa kuwekeza kwa mujibu wa utaratibu na kwamba suala la wachuuzi watalisimamia kwa nguvu kubwa, ili kazi hiyo iweze kufanywa na wazawa.

Amesa baada ya wiki mbili akishapata orodha hiyo atajua nini cha kufanya, kwani wawekezaji wanahitajika kuwekeza kwenye viwanda, kutoa ajira kwa Watanzania.Amesema katika kufuatilia kero na changamoto za wafanyabiashara na wenye viwanda atatoa namba maalum ya simu, ili kushughulikia masuala hayo kwa umakini mkubwa, lengo likiwa ni kufikia hatua ambayo wapo watakaoshukuru kwa changamoto kumalizika.

Kuhusu soko la Kariakoo kufanya biashara kwa saa 24, ameitaka Halmashauri ya Jiji kuweka mikakati ya muda mrefu na mfupi kuhusu uboreshaji wa biashara katika eneo la Kariakoo kwamba ni barabara zipi zifungwe, ili kuruhusu biashara kufanyika kwa saa 24.

“Soko lina heshima kubwa hivyo natamani Kariakoo yenye sifa zake kwamba magari yawe kwenye msongamano wakipakia mizigo na sio sehemu ya vurugu,” amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji, Jomaary Satura amesema katika kuboresha biashara kwa jiji hilo wamejipanga kujengo jengo la gorofa tano katika soko la Mchikichini na kuwa soko la wazi, ambapo kiasi cha Sh bilioni 48 kinatarajiwa kutumika.

Amesema wanatarajia kutoa Sh bilioni 30 kwa soko la Ilala kwa ajili ya uboreshaji zaidi na pia kuiwezesha Kariakoo kufanya biashara kwa saa 24 kwa kuweka taa pamoja na kamera kwa ajili ya usalama zaidi.

Katibu wa Wafanyabiashara Kanda ya kaskazini, Ismail Masoud amemkaribisha Waziri Jaffo katika familia ya wafanyabiashara aliyosema ni muhimu katika kuinua uchumi wa nchi.

Amemueleza kuwa ni muhimu kufuatilia matatizo ya wafanyabaishara hao hususani  suala la kodi, kwa kuwa Kariakoo ikidhurika uchumi wa nchi nao utaporomoka.

Amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uteuzi wa Waziri huyo na kwamba wako tayari kumpa ushirikiano.



0/Post a Comment/Comments