MAMBO SABA YA KUJIULIZA KABLA YA KUKOPESHA


*********

 Na (JUSTINE KALEB - 0755545600/0713636264)

Kukopesha ni kitendo cha kumpa mtu, kikundi cha watu au taasisi kiasi fulani cha fedha au mali kwa makubaliano ya kurejesha fedha hizo baada ya muda zikiwa pamoja na riba au kama jinsi zilivyo. Pia kukopesha ni kuazimisha mali au fedha kwa mtu ambaza atawajibika kurejesha ndani ya muda mliokubaliana kwa masharti mliyokubaliana. 


Kukopesha huleta ladha nzuri ya mafanikio kifedha wakati wale wanaokopeshwa wanapokuwa waaminifu kurejesha fedha hizo kwa wakati. Kukopesha hukuza mtaji kwa haraka, hulinda thamani ya pesa yako na huongeza mzunguko wa pesa na kukuza uchumi. Huwafanya watu kutimiza malengo yao na huwa chanzo cha mitaji kwa watu wengine na kuvutia faida kubwa ndani ya muda mfupi. 

Kutorejeshwa kwa fedha hizo za mkopo ndani ya muda mliokubaliana na mkopaji huleta ishara ya aidha kutolipwa kabisa fedha hizo au kulipwa nje ya muda ambapo thamani yake itakuwa imeshuka tofauti na mlivyokubaliana hapo awali. Kutorejeshwa kwa mkopo huleta hasara, huchelewesha kutimia kwa malengo ya mkopeshaji, huvunja mahusiano mazuri ya kibiashara yaliyojengwa kwa muda mrefu kati ya mkopaji na mkopeshaji na mkopeshaji asipokuwa mwangalifu anaweza kufilisika kwa sababu ya kukopesha watu ambao hawalipi.

Kukopa harusi, kulipa matanga ndio msemo unaoweza kukupa taswira nzuri ya mambo gani ujiulize kabla ya kukopesha. Wengine hujifariji kuwa mdaiwa hafungwi, kwa hiyo wanaweza wasikulipe na wasipate madhara yoyote kisheria, lakini wanajidanganya tu maana mdaiwa anaweza kufungwa. Sheria ya mwennendo wa Kesi za Madai, SURA 33 ya 2002 katika Jedwali la Kwanza, Kifungu cha XXI Kanuni ya 35 na 36 kwamba, mdaiwa anaweza kufungwa endapo atashindwa kulipa deni na ikiwa mdai ataiomba mahakama imfunge mdaiwa na atakuwa tayari kugharamia gharama zake awapo gerezani. Hivyo mahakama baada ya kujiridhisha inaweza kuamuru mdaiwa akamatwe afungwe kama mfungwa wa madai (civil prison).

Usipokuwa makini kabla ya kukopesha unaweza ukajikuta unafirisika, unagombana na watu, ndoa yako inavunjika, undugu unaisha na urafiki uliodumu kwa muda mrefu unavunjika. Hii ni kwa sababu tu umeshindwa kujenga mazingira mazuri ya uwajibikaji kisheria kati yako na yule unayemkopesha. Hii haijalishi unamkopesha nani na kiasi gani unachokopesha. 

Mali bila daftari hupotea bila habari. Ukishindwa kuweka kumbukumbu zako vizuri utapoteza pesa nyingi pasipo kujua na hatimaye kufilisika. Fedha haina undugu, ujamaa, kujuana wala urafiki. Ukitaka kufanikiwa kifedha na kudumisha mafanikio yako, lazima ujenge misingi imara ya kisheria itakayolinda fedha zako na kulinda maslahi ya vizazi vijavyo. Hivyo usikopeshe kwa kuangalia leo, bali kopesha kwa kuangalia kesho. Usiwe na maono ya kuku bali kuwa na maono ya tai yenye uwezo wa kuona miaka mingi ijayo na kuchukua tahadhari mapema iwezekanavyo.

Kwanza jiulize; je kuna mkataba wa maandishi kati yako na yule unayemkopesha? Hii ina maana usimkopeshe mtu kwa makubaliano ya mdomo tu. Hii haijalishi unamuamini kiasi gani. Katika maswala ya kifedha usimuamini mtu kupita kiasi, atakuja kukushangaza atakapokugeuka na kukuliza.  

Pili jiulize je, mkataba huo umeshuhudiwa na wakili, hakimu au shahidi mwingine yeyote? Ni muhimu kuwa na mtu wa tatu kama shahidi katika mkataba wenu, atasaidia kuutetea mkataba huo. 

Tatu jiulize, je mtu huyo anayeingia mkataba huo ana mamlaka kisheria ya kuingia mkataba huo na je ndiye atakayewajibika katika urejeshwaji wa mkopo huo? Usije ukaingia mkataba na mtu mwingine na ukatarajia ulipwe na mtu mwingine, utakwama. 

Nne jiulize, unafahamu anwani sahihi ya huyo unayemkopesha kwa maana ya anapoishi, ofisi yake, mawasiliano yake, mjumbe wake na mengineyo? Usimkopeshe mtu ambaye mmekutana tu barabarani, kanisani au msikitini. Siku akiacha kupita hiyo njia au kuja kwenye ibada umepoteza fedha zako. Fahamu nyumbani kwake, majirani zake na kiongozi wake wa serikali, mwajiri wake na ikiwezekana wafanyakazi wenzake.

Tano jiulize, je mtu huyo ana uwezo wa kulipa fedha hizo alizokopa ndani ya muda mliokubaliana? Usimkopeshe mtu kwa kumhurumia ili atatue shida zake tu, kopesha kwa maslahi ya kibiashara. Kama unajua kabisa mtu huyo hana uwezo wa kulipa pesa hizo ni bora usimkopeshe kuliko ukajiingiza kwenye migogoro isyokuwa ya lazima.

Sita jiulize, je mtu huyo ana dhamana yoyote ya mkopo huo au kuna mtu amejitolea kumdhamini ambaye asipolipa yeye ana uwezo wa kulipa deni hilo? Kukosekana kwa dhamana au mdhamini ni kuhatarisha ulinzi na usalama wa fedha zako. 

Saba jiulize, endapo mtu huyo akifariki, akipata ulemavu wa kudumu au tatizo na hivyo kushindwa kurejesha mkopo huo utawezaje kurejesha fedha zako? Ukiona hupati majibu, tafakari mara mbili kabla hujakopesha.

Haya ni mambo ya msingi sana ya kujiuliza na kuyapatia majibu kwanza kabla hujatoa fedha zako kumkopesha yeyote yule. Ukiona huna majibu sahihi ya maswali hayo usithubutu kumkopesha mtu fedha. Sio lazima mkopeshe kila mtu, watu wengine ili muendelee kuwa na mahusiano nao mazuri inabidi usiwakopeshe. Hakikisha umeweka ulinzi wa kutosha wa fedha zako kurudi na faida kabla hujakopesha.

Bora lawama kuliko fedheha. Hata kama utalaumiwa lakini fedha zako zitakuwa salama. Kwa taasisi zinazotoa mikopo ni muhimu kupata vibali vinavyokuruhusu kufanya hivyo na pia kulinda haki za mteja kisheria kwa kutomdharirisha, kumnyanyasa na kumfanyia fujo kwa sababu tu ameshindwa kuleta marejesho. Kumbuka kudaiwa hakumuondolei
mtu haki zake za msingi kisheria.

0/Post a Comment/Comments