Mwonekano wa shule ya sekondari(haihusiani na shule iliyotajwa kutokuwa na mwalimu wa kike)
Madiwani wakiwa kwenye kikao chao cha uwasilishaji wa taarifa za Kata.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Leo Rushahu,akiongea jambo na madiwani
.....................
Na Daniel Limbe,Biharamulo
UHABA mkubwa wa watumishi kwenye halmashauri ya wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera umesababisha baadhi ya wanafunzi wa kike kushindwa kuhudhuria vyema masomo yao kutokana na shule ya sekondari Rwagati kutokuwa na mwalimu wa kike hata mmoja.
Licha ya shule hiyo kuwa na walimu 16 wanafunzi wa kike 314 na wavulana 375 haina Mwalimu wa kike ambaye anaweza kuwahudumia wanafunzi wa kike kutokana na hali halisi ya kimaumbile ambapo hali hiyo imekuwa ikisababisha wanafunzi hao kukaa nyumbani na kuambulia adhabu kwa walimu wao baada ya kurejea shuleni.
Diwani wa Kata ya Runazi,Aniceth Bruzo,amesema hayo kwenye kikao cha Baraza la madiwani, wakati akiwasilisha taarifa za kata yake kwenye kikao cha robo ya nne, ambapo amesema changamoto hiyo imekuwa ikiwanyima uhuru wanafunzi na kwamba kukosekana kwa walimu wa kike ni sawa na kuwatendea ukatili wa kijinsia wanafunzi hao.
Amesema watoto wa kike ni muhimu wakathaminiwa kwa kupatiwa walimu ambao wanaweza kuwa washauri wa masuala ya kijinsia ikiwemo ugawaji na utumiaji wa taulo za kike.
"Ifike mahali tuwaonee huruma wanafunzi wa kike,shule haina mwalimu wa kike watoto wanashindwa wamweleze nani masuala yao kwa kuwa waliopo wote ni wakiume,hamuoni kama huo ni ukatili wa kijinsia katika elimu na wengine wanaambulia adhabu ya viboko kutokana na utolo wanaporejea shuleni,kitendo unacho weza kusema ni ukatili wa kimwili" amesema Bruno.
"Niombe kupitia kikao cha baraza hili shule ile ipelekewe Mwalimu wa kike ili tusaidie kukuza taaluma ya wanafunzi wetu,vinginevyo utolo utaongezeka na huenda baadhi ya wanafunzi wakaamua kuhama maeneo hayo".
Akijibu malalamiko hayo,Kaimu Ofisa elimu sekondari wilayani humo,
Domistian Bajumuzi, amesema suala hilo litashughulikiwa haraka ili kuondoa adha inayowakabili wanafunzi hao.
Hata hivyo mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Leo Rushahu,amesisitiza kutatuliwa changamoto hiyo haraka kwa kuwa ni aibu kwa shule kukosa Mwalimu wa kike huku akisisitiza suala ya matumizi ya mashine za POS katika ukusanyaji mapato ya halmashauri hiyo.
Vilevile ametumia fursa hiyo kuwaonya wenyeviti na watendaji wa vijiji kuacha mara moja matumizi ya pesa mbichi badala yake pesa zote zinapaswa kupitia mfumo wa benki ili kuwe na uratibu mzuri wa utekelezaji wa miradi
Post a Comment