DAWASA YATEKELEZA HUDUMA YA MAJI KWA WANANCHI WA MSUMI NA KIBAHA

 Ni mpango wa muda mfupi kufikisha huduma ambayo miradi mikubwa ya Maji inaendelea kutekelezwa


Umewahi kujiuliza gharama za upatikanaji wa huduma za Majisafi kwa Maeneo ambayo hayana mtandao rasmi wa mabomba?

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeanza kuchukua hatua za muda mfupi kwa maeneo ambayo hayana mtandao wa Maji kwa kuwapelekea huduma ya Maji na kuyasambaza kwa Wananchi kwa gharama nafuu.

Huduma hiyo imeanza kwa Wakazi wa Ubungo ,Tabata na Kibaha katika Mitaa ya Msumi A, B ,C na Tabata katika mitaa ya Kajima, Novo, Vingunguti Faru na Kipawa na kwa upande wa Kibaha katika maeneo ya Boko Mnemela, Viziwaziwa na Muheza ili kuwahudumia wakazi wa maeneo hayo

Akizungumza wakati wa zoezi la usambazaji huduma hiyo, Mkurugenzi wa Huduma Kwa Wateja DAWASA, CPA (T) Rithamary Lwabulinda amesema kuwa Mamlaka inaendelea na juhudi za kuhakikisha inapunguza changamoto ya muda mfupi ya maji kwa Wakazi kwa kuwasogezea huduma huku mipango ya baadae ya kusogeza huduma ikiwa mbioni kwa utekelezaji wa miradi mingine mikubwa maeneo mbalimbali.

"DAWASA imebainisha maeneo yanayohitaji hatua za awali wakati mipango mikubwa ya kusambaza miradi ikiendelea. Tumeanza kusambaza huduma hii na hadi sasa tumesambaza katika maeneo ya Msumi A, Darajani, Kwa Panya na Msumi Stendi ambayo kupitia hayo itasaidia kupunguza gharama za maisha pamoja na kuongeza tija ya muda katika kufanya shughuli nyingine za uzalishaji na kukuza kiuchumi." Amesema Lwabulinda

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Msumi, Ismail Agostini Mbinda ameishukuru Serikali na DAWASA kwa ushirikiano wa kuhakikisha wakazi wa Msumi wanaimarishiwa huduma ya majisafi.

"Wana-Msumi sasa wana shangwe na furaha kwa kuona ndoto zao za kupata majisafi na salama zinatimia baada huduma ya maji ambayo watakuwa wakichangia gharama ndogo za Shilingi 50 kwa ndoo ya ujazo wa lita 20 badala ya Shilingi 500 hadi 700 walizokuwa wakinunua kwa wauzaji binafsi". Amesema

Naye mmoja wa wakazi wa Mtaa wa Msumi A, Catherine Joseph amesema kuwa kupitia mpango huu itawapunguzia adha kubwa ya kutumia muda mwingi kutafuta maji na kuwapunguzia makali ya kununua huduma ya Maji kwa gharama kubwa.

"Tumefurahi sana na tunaishukuru DAWASA kwa jambo hili linatupunguzia kero ya kuamka usiku wa manane kwenda kuhemea maji ambapo wakati mwingine hugombana kupigania maji, tunaamini sasa kadhia hiyo itaisha kabisa." Amesema Catherine.




0/Post a Comment/Comments