TANESCO TEMEKE YAGUSA MAISHA YA WATEJA WAKE

Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke Mhandisi Ezekiel Mashola akimkabidhi Zawadi ya Jiko Janja linalotumia Nishati ya Umeme mteja wake Mkazi wa Yombo Vituka Bi. Brigitha Mrope wakati walipomtembelea leo Oktoba 9, 2024 nyumbani kwake jijini Dar es Salaam, katikati ni Diwani wa Kata ya Yombo Vituka Fulgence Rwiza. (PICHA NA NOEL RUKANUGA)
Wafanyakazi wa TANESCO Mkoa wa Temeke wakimfundisha mteja wao Bi. Brigitha Mrope jinsi ya kutumia jiko janja linalotumia nishati ya umeme.
Mteja wa TANESCO Mkoa wa Temeke Bi. Brigitha Mrope akionesha eneo analopikia kupitia kuni.
Wafanyakazi wa TANESCO Mkoa wa Temeke wakiwa katika picha ya pamoja na Mteja wao Bi. Brigitha Mrope baada ya kumkabidhi zawadi ya jiko janja
Diwani wa Kata ya Yombo Vituka Fulgence Rwiza akifafanulia jambo wakati Wafanyakazi wa TANESCO Mkoa wa Temeke wakiwa Nyumbani kwa mteja wao Bi. Brigitha Mrope katika Mtaa wa Sigara.
Wafanyakazi wa TANESCO Mkoa wa Temeke wakielekea Nyumbani kwa Mteja wao kwa ajili ya kumpatia Zawadi ya Jiko janja linalotumia Nishati ya Umeme.
...........
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke limerudisha faida kwa jamii kwa kutoa jiko janja ambalo linatumia nishati ya umeme kwa Mteja wake Mkazi wa Yombo Vituka Bi. Brigitha Mrope kwa ajili ya kumsaidia kuacha matumizi ya kuni ambayo yamemsababishia matatizo ya kiafya.
Akizungumza leo Oktoba 9, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akikabidhi Jiko Janja nyumbani kwa Mteja Bi. Brigitha Mrope, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Temeke Mhandisi Ezekiel Mashola, amesema kuwa katika kusherekea wiki ya huduma kwa wateja wameamua kufanya matukio mbalimbali ikiwemo kuwatembelea wateja wao kutoa elimu pamoja na kurudisha faida.
Mhandisi Mashola amesema kuwa “leo tumekuja kumletea mteja wetu zawadi ya jiko janja ambalo linatumia nishati ya umeme kwani alikuwa anapata changamoto nyingi, pia hii ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suruhu Hassani ya kutumia nishati safi”
Amefafanua kuwa jiko hilo lina uwezo wa kuivisha chakula kwa haraka kwa kutumia uniti moja ya umeme yenye thamani ya shilingi 350, huku akieleza kuwa lengo ni kuhamasisha matumizi ya nishati safi.
Aidha, Diwani wa Kata ya Yombo Vituka Bw. Fulgence Rwiza, ameushukuru uongozi wa TANESCO Mkoa wa Temeke pamoja na wafanyakazi kwa kuona umuhimu wa kurudisha faida kwa jamii kwa kutoa jiko janja linalotumia uniti chache za umeme.
Amesema kuwa kilichofanywa na TANESCO ni mfano ya kuigwa kwa Taasisi nyengine kwa kurudisha faida kwa jamii, huku akisisitiza umuhimu wa kutumia nishati safi.
Nae, Afisa Mtendaji mtaa wa Sigara Bwana James Mgonja amesema, "Nashukuru kwa kuwagusa wateja wenu wenye hali ya chini kiuchumi, naomba muendelee kutekeleza kwa vitendo kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya umeme” amesema Bw. Mgonjwa.
Kwa upande wake Bi. Brigitha Mrope ameushukuru uongozi wa TANESCO kwa kumsaidia kumpatia zawadi ya jiko janja linalotumia nishati chache ya umeme kwa ajili ya matumizi ya kupikia.
Amesema kuwa awali alikuwa anapikia kuni pamoja na mkaa ambao umemletea shida ya kiafya, hivyo jiko hilo litakuwa msaada mkubwa kwake katika kubana matumizi na kuepukana na magonjwa yanayotokana na matumizi ya nishati ambayo sio rafiki.

0/Post a Comment/Comments