Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewahimiza waajiri nchini
kuongeza umakini na kuzingatia misingi ya utu mahali pa kazi ili iwe motisha na
chachu kwa watumishi kuongeza ubunifu na ufanisi kazini.
Dkt. Biteko
amesema hayo wakati akimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Phillip Mpango katika usiku wa Tuzo kwa mwajiri Bora wa
mwaka 2024 ambapo Kampuni ya bia nchini (TBL) imeibuka mshindi wa jumla
ikifuatiwa Kampuni ya Barick Gold huku Mamlaka ya Bandari Tanzania TPA ikishika
nafasi ya tatu.
Amewapongeza
waandaaji wa tuzo hizo na kuwataka kupanua wigo wa makundi ya ushiriki huku
akisisitiza umuhimu wa utoaji wa motisha mahala pa kazi ili watumishi waongeze
ari ya kufanya kazi kwa viwango na ubora wajuu.
“ mwajiri
anachokihitaji kwa mwajiriwa ni muda na ujuzi wake basi. Hivyo, waajiri
ongezeni umakini na utu mahali pa kazi na mkifanya hivyo, waajiriwa ambao
wanatumia muda mwingi kazini, wataongeza ubunifu na ufanisi na kuleta tija ya
kazi,” amesema Dkt. Biteko
Aidha, Dkt.
Biteko ameongeza kuwa Serikali inatambua mchango wa ATE katika maendeleo na
program mbalimbali za maendeleo ikiwemo suala la ukuzaji wa uwiano wa kijinsia
mahali pa kazi.
Akimkaribisha
mgeni rasmi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na wenye
ulemavu, Mhe. Ridhiwan Kikwete amesema Serikali kwa kushirikiana na Chama cha
waajiri Tanzania (ATE) na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini TUCTA
imeongeza makundi ya ushiriki kwa waajiri ikiwemo kigezo cha utambuzi wa watu
wanaoishi na Virusi vya Ukimwi pamoja na mwajiri anaezingatia masuala ya usawa
wa kijinsia katika uajiri.
Ameongeza
kuwa kwa msingi huo, Tanzania inajitanabaisha kimataifa kwa kuwa na Kiongozi
Mkuu mwanamke (Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan) suala ambalo amesema
linaiweka nchi katika nafasi ya juu kimataifa katika masuala ya usawa wa
kijinsia.
Naye
Mtendaji Mkuu wa ATE, Suzan Ndomba amesema tangu kuasisiwa kwa tuzo za mwajiri
bora wa mwaka miaka 19 iliyopita washiriki wamekuwa wakiongezeka na kuongeza
ufanisi na waajiri kuboresha mazingira ya kazi.
Kwa upande
wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Kanda ya Afrika
Mashariki, Caroline Mugalla amepongeza hatua iliyofikiwa katika utoaji wa tuzo
hizo, ameshauri mashindano hayo pia yahusishe na kutambua shughuli za vijana
katika sekta isiyo rasmi ambayo ina mchango mkubwa katika jamii.
“Ni muhimu kuangalia namna ya kutambua mchango wa sekta isiyo rasmi ili kuweza kupata ajira zenye staha, amesema Mugalla.
=MWISHO=**
Post a Comment