JELA MIAKA 20 KUKUTWA NA MENO YA TEMBO,BUNDUKI

 

******


Na Daniel Limbe,Biharamulo

MAHAKAMA ya wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera imemhukumu kutumikia kifungo cha miaka 20 jela, Raphael Daud (44) baada ya kupatikana na nyara za serikali pamoja na kumiliki silaha kinyume cha sheria.

Mshitakiwa huyo,ambaye ni mkazi wa kijiji cha Nyamaragala kata ya Rusahunga wilayani humo,alishitakiwa kwa makosa mawili tofauti baada ya kudaiwa kukamatwa na meno mawili ya tembo pamoja na kumiliki silaha aina ya gobole.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu mkazi mkuu wa mahakama ya wilaya ya Biharamulo,Frola Ndele,baada ya kuridhika na ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashitaka pasipo kuacha shaka.

Kabla ya kusoma hukumu hiyo,mshitakiwa alipewa fursa ya kuomba kupunguziwa adhabu,ambapo alidai anafamilia inayomtegemea na kwamba iwapo atafungwa itateseka kwa sababu yeye ndiyo chanzo cha kipato cha familia.

Awali mwendesha mashitaka kutoka Ofisi ya mashitaka wilaya ya Biharamulo, Wakili Edith Tuka,akishirikiana na Suddy Lugano,waliieleza mahakama hiyo kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo kwa makusudi huku akijua wazi kuwa kumiliki meno ya tembo na silaha ya moto ni kinyume cha sheria za nchi.

Na kwamba baada ya mshitakiwa kukamatwa februali 2, 2023 na kikosi maalumu cha kudhibiti ujangili kwenye hifadhi ya taifa ya Burigi-Chato,aliwaongoza kwenda porini kuwaonyesha alipoficha nyara hizo pamoja na silaha (Gobole) ambalo hutumika kwaajili ya kuuwa wanyamapori.

Akitoa hukumu hiyo,Frola amesema kitendo cha kukutwa na nyara za serikali ni kinyume na kifungu cha 86(1) na (2)(c)(iii) cha sheria ya uhifadhi wanyamapori namba 283 ya mwaka 2002 ikisomwa pamoja na aya ya 14 jedwali la kwanza na kifungu cha 60(2) cha sheria ya kudhibiti uhalifu wa kiuchumi namba 200 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Ambapo kosa la pili ni kinyume na kifungu cha 20(1)(a) (b) na 2 cha sheria ya kudhibiti silaha na vilipuzi namba 2 ya mwaka 2015 ikisomwa pamoja na aya ya 31 jedwali la kwanza pamoja na kifungu cha 60(2) cha sheria ya uhujumu uchumi namba 200 ya mwaka 2022.

Baada ya ufafanuzi huo,mahakama ikafikia uamuzi wa kumfunga miaka 20 jela ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye nia ya kutenda makosa kama hayo.

Hata hivyo,mshitakiwa amepewa haki ya kukata rufaa iwapo hakuridhika na uamuzi uliotolewa na mahakama hiyo,huku askari waliokuwa mahakamani hapo wamemchukua na kumpeleka kwenye gereza la wilaya hiyo kuanza kutumikia kifungo chake.

                           Mwisho.


0/Post a Comment/Comments