MKAKATI WA UTEKELEZAJI WA SERA YA MALIKALE, LANGO LA FURSA ZA UTALII.

.......................

Na Sixmund Begashe – Dodoma

Serikali ya awamu ya Sita chini ya  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendeleza jitihada za  uhifadhi endelevu na utangazaji wa malikale nchini kwa kuandaa Mkakati wa utekelezaji wa Sera ya Malikale ya mwaka 2008 ambao utatekelezwa kwa kushirikisha wadau mbalimbali.

Akifungua kikao kazi cha  wadau cha kujadili Mkakati wa Utekelezaji wa Sera hiyo, Jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Uhifadhi, Kamishana wa Polisi Benedict Wakulyamba, amesema utalii wa kihistoria hapa nchini umekuwa kwa kasi hivyo uwepo wa Sera na Mikakati hiyo  itawezesha Sekta ya Malikale kunufaisha nchi na wadau wake.

CP. Wakulyamba ameongeza kuwa kutokana na jitihada hizo za  Mhe. Rais Dkt.  Samia  za kuendeleza sekta ya Utalii nchini, ni wazi Sera na Mikakati huo itasaidia  sekta ya Utalii wa Mali kale kulinufaisha Taifa na wadau wake na kuongeza kua kushirikisha wadau kupitia Mkakati huo kutasaidia kuondokana na changamoto zinazoikabili sekta  hiyo.

‘‘Uharibifu wa malikale, mabadiliko ya tabianchi, wadau kutoshirikishwa ipasavyo zinapaswa kujibiwa na mkakati huu. Mkakati ukiandaliwa ipasavyo utaweza kujibu hoja za msingi ambazo zitaleta tija katika Sekta hii ya Malikale.’’ CP. Wakulyamba.

Aidha CP. Wakulyamba ametoa rai kwa jamii kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuthamini na kuhifadhi utajiri wa urithi wa Historia na Malikale nchini ili uweze kuendelea kuwanufaisha watanzania wote na kwa maslahi mapana ya kizazi kinacho kuja.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Malikale, Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Uhifadhi wa Malikale Dkt. Emmanuel Bwasiri amesema makakati huo utatekelezwa kwa miaka kumi 2024 – 2025 na utazingatia mambo muhimu ikiwemo kutoa  elimu kwa umma na uhamasishaji, kufanya tafiti na uhifadhi, umairishaji wa Taasisi na kukuza Ushirikiano wa Kimataifa.

Naye Mhadhiri wa Akiolojia na Malikale, Idara ya Historia na Akiolojia, Chuo kikuu Cha Dodoma, Dkt. Abel Shikoni licha ya kuipongeza serekali kwa kushirikisha wadau kwenye kuunda mkakati huo, amesema pamoja na mambo mengine  utekelezaji wake  utafungua fursa za ajira kwa watanzania hususani wahitimu wa vyuo vikuu nchini.

0/Post a Comment/Comments