Makamu Mkuu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Prof. Appolinary Kamuhabwa ( wa pili kulia) Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Ntuli Kapologwe (wa pili kushoto) wakiongoza mbio za Fund runs awamu wa tatu (season three) ambazo zina lengo la kuchangia ujenzi wa uwanja mazoezi kwa ajili ya jumuiya ya wanafunzi,wafanyakazi wa Chuo na wafanyakazi na jamii kwa ujumla.
****
Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
WAKATI magonjwa yasiyoambukiza yakiendelea kuwa tishio nchini Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (Muhas) kimeanzisha mapambano ya kuyadhibiti magonjwa hayo nje ya hospitali.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Appolinary Kamuhabwa amebainisha hayo leo Novemba 23,2024 Jijini Dar es Salaam wakati wa mbio za uchangiaji wa uwanja mazoezi kwa ajili ya jumuiya ya wanafunzi,wafanyakazi wa Chuo na wafanyakazi wa hospitali zilizopo jirani.
Mkuu huyo wa Chuo amebainisha kuwa uwanja huo utakuwa sehemu ya mapambano ya magonjwa hayo ambayo yanasababisha vifo na ulemavu.
"Mbio hizi tunazita Muhas Fund runs session 3 hapa Muhimbili kama mnavyojua sisi chuo cha afya ambao tunatoa mafunzo ya afya tunafanya utafiti wa afya lakini vilevile tunatoa huduma ya afya kwa hiyo linapokuwa suala la mazoezi sio suala la kuimarisha tu mwili ni suala la kiafya"
Amesema kuwa ujenzi wa uwanja huo umechagizwa na kasi ya kuenea kwa magonjwa yasiyoambukiza.
"Kama mnavyojua sasa hivi kwa nchi yetu na duniani kuna ongezeko kubwa la maradhi yasiyoambukiza kama saratani , kisukari, Shinikizo la damu na maradhi mengine yasiyoambukiza .
Ametaja moja sababu moja wapo ya kisababishi kikubwa Cha magonjwa hayo ni watu kuwa mtindo mbaya wa maisha ikiwemo kutofanya mazoezi.
"Tunaona tukiwa na kituo hiki ni muhimu kwa wananchi wa Dar es Salaam, wanafunzi pamoja na wagonjwa wale ambao wametibiwa sasa wameanza kurudisha afya zao.Kituo hiki kinaweza kutumika katika kuboresha afya zao.
Amesema kuwa uwanja huo utakuwa na sehemu ya uwanja wa Mpira wa Miguu, mpira wa Mikono na sehemu ya kuoga na kubadilisha nguo pamoja na ile sehemu ya mazoezi ya viungo(gym).
"Tuna uwanja wetu tayari tumetafuta wataalam ambao wameusanifu tunaweza tukawa tuna uwanja wa mpira wa miguu netball na Basketball. Jengo dogo kwa ajili ya kuoga na kubadilisha nguo kwa juu tukajenga Gym tunaona hiki ni kituo muhimu sana kwa kutekeleza mujukumu yetu ya kufundisha tafiti na kutoa huduma za afya," amesema Profesa.
Amesema kuwa viwanja hivyo vitawanufaisha wafanyakazi wa Hospitali ya Muhimbili, Taasisi ya Mifupa (Moi) Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ,wanafunzi wa Muhas na wafanyakazi wa chuo hicho , wananchi wa Dar es Salaam na wagonjwa watakaokuwa na nafuu na wenye kuhitaji mazoezi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Ntuli Kapologwe, amesema kuwa mbio hizo zinaendana na kampeni ya kitaifa ya Mtu ni Afya.
“Mbio hizi siyo tu zinahamasisha mazoezi, bali pia zinasaidia kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu, kisukari, na magonjwa ya moyo. Hii ni sehemu ya kampeni ya Fanya Kweli Usibaki Nyuma inayolenga kuhakikisha kila mtu anajali afya yake,” amesema Dkt. Kapologwe.
Naye, rais wa MUHAS, Marsha Macatta-Yambi mhitimu wa Chuo hucho, amesema kuwa ndoto ya chuo ni kutengeneza uwanja huo itawasaidia wanajamii kuhamasika kufanya mazoezi na kujilinda na maradhi nyemelezi.
"Sisi tunaona ni fahari sana kwa ndoto hii nzuri na yenye maana kwa kutengeneza sehemu itakayowasaidia wanajamii wa hapa ni jambo la kisasa na lenye kuendana na changamoto zilizopo.
Maisha yetu yamekuwa yanaendeshwa na mambo mengi tunaweza kufika saa 24 bila kufanya mazoezi"
Amesema kuwa kiwanja hicho kitasaidia hamasa ya vitendo kwa jamii pale ambapo wataalam wa afya wakihamisha mazoezi .
"Hili litasaidia afya zetu lakini pia litatoa taswira ya uhalisia tukiwa tunahamasisha mazoezi"
Wanafunzi nao walionyesha mshikamano katika tukio hilo, ambapo Pendo Paul, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Shahada ya Uuguzi, alisisitiza umuhimu wa mazoezi kwa afya. “Mazoezi ni njia rahisi ya kuimarisha afya na kuepuka magonjwa, hivyo tunapaswa kuyafanya kuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku,” amesema.
Post a Comment