TAKUKURU (M) TEMEKE YATOA TATHMINI YA UTENDAJI KAZI JULAI-SEPT 2024

Naibu Mkuu wa TAKUKURU (M) Temeke Ismail Bukuku akizungumza na wanahabari wakati akitoa taarifa ya tathmini ya utendaji kazi kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka ya 2024/2025.
Wanahabari wakifuatilia mazungumzo ya Naibu Mkuu wa TAKUKURU (M) Temeke Ismail Bukuku wakati akitoa taarifa ya tathmini ya utendaji kazi kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka ya 2024/2025.

.......................

NA MUSSA KHALID

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke imepokea malalamiko 55 huku 50 yakihusu rushwa na matano hayahusu rushwa katika kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu.

Pia imesema licha ya kufanya mikakati na juhudi za kuzuia Rushwa bado wapo wananchi wachache ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo hivyo.

Hayo yameelezwa jijini Dar es salaam na Naibu Mkuu wa TAKUKURU (M) Temeke Ismail Bukuku wakati akitoa taarifa ya tathmini ya utendaji kazi kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka ya 2024/2025.

Awali Bukuku amesema TAKUKURU (M) Temeke katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2024/2025 imefanya ufuatiliaji wa miradi minne yenye thamani ya shilingi bilioni 11.7 ambayo mmoja kati ya hiyo unaotekelezwa Manispaa ya Temeke na Kigamboni huko miradi mitatu iliyobaki yenye thamani ya milioni 894 inatekelezwa katika Manispaa ya Kigamboni pekee

Katika kuhakikisha mapambano dhidi ya rushwa yanafanikiwa,Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Temeke kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2024/2025 ilishiriki katika maonesho 48 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu rushwa.

Aidha katika kutekeleza program ya TAKUKURU Rafiki, Bukuku amesema huwa wanaifanya katika kila kata kwa ajili ya kusikiliza kero mbalimbali kutoka kwa wananchi na kuweza kuzitatua.

Katika hatua nyingine,Naibu Mkuu huyo wa TAKUKURU (M) Temeke ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa watumishi wa Idara ya Ardhi Kigamboni kutoa huduma kwa wananchi wote bila kuwabagua kwa misingi yeyote.

Hata hivyo TAKUKURU imeendelea kuwasisitiza watanzania kuwa na mazoea ya kutoa taarifa dhidi ya vitendo au viashiria vya Rushwa kwenye maeneo yao ili kuweza kuvidhibiti kwa wakati.

0/Post a Comment/Comments