TIRA YAZINDUA TAARIFA YA UTENDAJI WA SOKO LA BIMA 2023

*****

Na Mwandishi wetu 

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imezindua taarifa ya utendaji wa soko la bima huku ikihimizwa kuimarisha matumizi ya teknolojia na kuhakikisha inafanya kazi kidigitali ili kwenda sambamba na kasi ya ukuaji. 

 Akizungumza kwenye uzinduzi wa taarifa hiyo ya mwaka 2023 Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande amesema sekta ya bima ina jukumu la kuhakikisha inasaidia kujenga uchumi na kuwapa wananchi ulinzi imara wa afya zao.

Katika eneo hilo, Chande aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo amesema hivi karibuni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha sheria ya 'Bima ya Afya' kwa wote ambayo kwa namna moja au nyingine inalenga kuona kila Mtanzania anakuwa na 'Bima ya Afya' hatua ambayo ameitaja kuwa ni kubwa na inayopaswa kuchangamkiwa na kila mmoja

Aidha, Chande amebainisha kuwa tafiti na tathmini mbalimbali zinaonesha kuwa soko la bima limekuwa likipanuka kukua kila siku na kwamba kwa taswira ya uzinduzi wa mwaka huu inaonesha wazi kuwa soko hilo litaendelea kukua zaidi hivyo ni wakati muafaka sasa kwa TIRA kujipanga kikamilifu na kuhakikisha inaenda sambamba na ukuaji wa soko

TIRA pia imetakiwa kusimama mstari wa mbele na kuhamasisha uwekezaji, sambamba na kuhakikisha sekta ya bima inaendelea kuimarika maradufu.

Hiyo, kwa mujibu wa Naibu Waziri Chande amesema inapaswa kwenda sambamba na mamlaka hiyo kugeukia fursa za bima zilizopo kwenye sekta ya michezo nchini, sekta ambayo ameitaja kuwa inakua kwa kasi hivyo ni vyema ukafanyika utafiti ili kuona namna bora ya kuwafikia wadau wa michezo kwa ujumla wake

Ametumia nafasi hiyo, kutoa pongezi kwa Shirikisho la Soka hapa nchini (TFF) na Benki ya Biashara ya NBC ambao ni wadhamini wakuu wa ligi kuu soka Tanzania Bara (NBC Premiere League) kwa kuanzisha mchakato wa mazungumzo na baadhi ya makampuni ya bima na kuingianao mikataba na kampuni hizo

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi na wadau mbalimbali kutoka taasisi za umma na sekta binafsi akiwemo Mwenyekiti wa Mabalozi wa Bima Tanzania ambaye pia ni Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Mhandisi Zena Ahmed Saidi, Waziri wa zamani wa Kilimo nchini ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Vwawa (CCM) na Balozi wa Bima Tanzania Japhet Hasunga nk

TIRA pia imetumia hafla hiyo kutoa tuzo kwa wadau na taasisi mbalimbali wanazofanyanao kazi kwa karibu au zinazofanya kazi zinazohusu bima na kutoa ushirikiano wa karibu kwao ikiwemo TRA, Jeshi la Polisi, Ofisi ya DPP, wanahabari, Mabalozi wa Bima.










0/Post a Comment/Comments