Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)Bw. Yusuph
Mwenda, ametoa onyo kali kwa wafanyabiashara wachache wanaojihusisha na
ukwepaji kodi kupitia mauzo hewa na risiti bandia.
Akizungumza Ijumaa, Desemba 20, 2024, wakati wa ziara yake
ya kuwashukuru walipakodi katika Soko la Kariakoo, Mwenda amesema kuwa tabia
hiyo ni kosa linalohujumu uchumi wa nchi.
“Kuna wachache wanakwepa kodi kwa kufanya mauzo hewa,
wanaonesha wamemuuzia mtu bidhaa za thamani kubwa wakati hawajafanya mauzo
hayo, risiti hizi bandia zinatumika kupunguza malipo ya kodi yanayostahili
kulipwa" CG Mwenda.
"Tunawajua wanaofanya hivyo, na vyombo vyetu
vinaendelea kufuatilia, Wito wangu ni kwamba waache mara moja, vinginevyo
watakamatwa na watahitajika kulipa kodi pamoja na riba na penati,” amesema
Mwenda.
Amewahimiza wafanyabiashara wa Kariakoo kuhakikisha wanatii
sheria za kodi na kuepuka kujihusisha na ununuzi wa risiti hizo bandia,
akisisitiza kuwa TRA imeimarisha mifumo yake ya ufuatiliaji ili kudhibiti
ukwepaji kodi kwa ufanisi.
Nao wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo wamepongeza juhudi
za TRA katika kuwaelimisha na kuwahamasisha kulipa kodi kwa njia rahisi na
salama. Bashiir Mohammed, mmoja wa wafanyabiashara, amesema:
“Sasa hivi kuna
uelewa wa kutosha, na kila mfanyabiashara amewezeshwa kufahamu namna ya kulipa
kodi kupitia mifumo ya TRA. Ninawashauri wenzangu tuwe waaminifu na tulipe kodi
bila kulazimishwa.”
Naye Peter Joseph amewasihi wafanyabiashara wenyewe kuwa
mstari wa mbele kulipa kodi bila kusubiri kufuatiliwa isipokuwa wanapofanya
biashara waatakiwa kwenda TRA kwa makadirio na kulipa kodi yao.
Ziara ya Kamishna Mkuu wa TRA katika Soko la Kariakoo
imelenga kuimarisha mahusiano kati ya mamlaka hiyo na wafanyabiashara, sambamba
na kusisitiza umuhimu wa kodi katika maendeleo ya nchi.
Post a Comment