DC CHATO AMWAGIZA MKANDARASI KUKAMILISHA BWENI MKUNGO

                      Bweni la wavulana shule ya sekondari Mkungo

Na Daniel Limbe,Chato

SERIKALI imemuagiza mkandarasi wa mradi wa Bweni la wavulana kwenye shule ya sekondari Mkungo wilayani Chato mkoani Geita kukamilisha uwekaji wa madirisha kabla ya januari 2025.

Hatua hiyo inalenga kuwanusuru watoto kutembea umbali mrefu ili kufika shuleni hapo, hali inayoweza kupunguza umakini wa kujisomea.

Akizungumza kwa nyakati tofauti katika ziara ya kukagua na kuihamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika uchangiaji wa aslimia 10 ya miradi inayofadhiliwa na mpango wa kunusuru kaya maskini nchini(Tasaf),Mkuu wa wilaya hiyo,Louis Bura,amesema hakuna sababu ya kuchelewesha miradi ya serikali iwapo fedha za utekelezaji zimeshatolewa.

Amesema mradi wa ujenzi wa bweni la wavulana mkungo upo katika hatua nzuri za kukamilika huku akimtaka mkandarasi kufanya kazi ya ukamilishaji wa madirisha kwa ufanisi kabla ya januari 2025 shule zitakapofunguliwa.

"Serikali imeleta fedha nyingi sana za ujenzi wa miradi ya maendeleo kwenye wilaya yetu ya Chato,wito wangu ni kuwataka wasimamizi wa miradi yote kujiepusha na tamaa ya fedha katika miradi hiyo".

Aidha ametumia fursa hiyo kuupongeza mradi wa kunusuru kaya maskini nchini (Tasaf) kwa kutoa fedha na kuwawezesha wananchi waliokuwa hawana uhakika wa kipato na kwamba baadhi yao sasa wamenufaika na ufugaji ikiwemo kuku na mbuzi.

"Niwaombe sana wote mnaosimamia miradi ya Tasaf muwe waaminifu na muwe na ushirikiano muda wote,maana mkianza migogoro mtakwamisha shughuli ambazo zimeelekezwa kuwanufaisha wananchi,kuweni na nidhamu ya fedha"amesema Bura.

Akizungumzia utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyofadhiliwa na mradi wa kunusuru kaya maskini wilayani Chato, kaimu mratibu wa Tasaf, Isaya Kimwagile,amesema yapo mafanikio makubwa sana kwa walengwa wa mpango huo ukilinganisha na awali.

Amesema hadi kufikia awamu ya tatu ya miradi ya Tasaf wilayani humo, wananchi wengi waliokuwa maskini wa vipato wamenufaika kwa fedha za moja kwa moja,kushiriki kwenye miradi pamoja na kupewa mifugo ili kujiendeleza kiafya na  kiuchumi.

Aidha baadhi ya wananchi maskini zaidi ambao hata walikuwa hawana sauti za kushiriki kwenye mambo ya kijamii ikiwemo mikutano ya hadhara,sasa wameweza kujitokeza,kuchangia mawazo yao pamoja na kushirikiana na wengine katika mambo mbalimbali tofauti na ilivyo kuwa awali.

Hata hivyo amesema,halmashauri inaendelea kusimamia miradi yote inayofadhiliwa na Tasaf kwa lengo la kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

Kadhalika mratibu huyo amesema mkandarasi anaetekeleza ujenzi wa bweni la wanafunzi 80 wa shule ya sekondari Mkungo pamoja na nyumba wa walimu(Two in One) tayari ameshapewa fedha zote za ukamilishaji mradi huo na kwamba kinachosubiriwa ni kupokea mradi kabla ya kuanza kutumika hapo mapema mwakani.

Baadhi ya wanufaika wa mbuzi kutoka kijiji cha Makurugusi,Anastazia Stephano na Rashid Ngoso,wameipongeza serikali kwa jitihada walizofanya katika kuwaondolea umaskini uliokithiri na kwamba sasa wanayo matumaini makubwa ya kupata milo mitatu kwa siku.

"Nampongeza sana rais Samia Suluhu Hassan,kwa kutujali sisi wananchi maskini mbuzi tulizopewa tunaendelea na ufugaji na manufaa yake tumeanza kuyaona,hakika serikali mmefanya jambo kubwa sana na ikiwezekana mtuongezee mbuzi wengine" amesema Anastazia.

    Mkuu wa wilaya ya Chato,Louis Bura,akizungumza na vyombo vya habari.
      Nyumba ya walimu shule ya sekondari Mkungo.

 Mkuu wa wilaya ya Chato,Louis Bura,akizungumza na vyombo vya habari.

                         Mwisho.

0/Post a Comment/Comments