Na Daniel Limbe,Chato
IKIWA ni miaka minne ya utawala wa rais Samia Suluhu Hassan madarakani, kamati ya amani wilaya ya Chato mkoani Geita imemhakikishia ushirikiano mkubwa kutokana na kuridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyoachwa na mtangulizi wake Hayati Dkt. John Magufuli.
Mbali na miradi hiyo, utolewaji wa fedha nyingi za maendeleo kwenye halmashauri ya wilaya hiyo pia ni miongoni mwa sababu kubwa za kuvutiwa na utawala wake ambao umesababisha miradi mingi ya maendeleo kukamilika kwa ubora wa hali ya juu huku mingine ikiendelea kujengwa.
Mwenyekiti wa kamati ya amani, ambaye pia ni shekhe wa wilaya hiyo, Abdurahman Ismail,amesema wanaridhishwa na namna rais Samia anavyoendelea kuwaletea wananchi maendeleo katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu,afya,maji,barabara, kilimo na uhifadhi wa mazingira.
Aidha katika tamko la kamati hiyo, wameipongeza halmashauri ya wilaya ya Chato kwa kusimamia vyema miradi mingi ya maendeleo ambayo baadhi yake ilikaguliwa na mbio za mwenge wa uhuru 2024 na kusifiwa kutokana na kuzingatia thamani halisi ya ujenzi wake.
"Nitumie nafasi hii kuipongeza halmashauri ya wilaya yetu kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo maana sisi kamati ya amani tumekuwa tukishirikishwa kikamilifu kuitembelea na kutoa ushauri wetu,vilevile tunamtia moyo rais wetu kuendelea kuchapa kazi badala ya kukatishwa tamaa na maneno ya mitandaoni" amesema Abdurahman.
Kwa upande wake mwenyekiti mwenza wa kamati hiyo, Mchungaji Zacharia Samson, ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuzidi kuihudumia wilaya hiyo kwa madai hakuna mradi uliosimama licha ya baadhi ya watu kuamini vinginevyo baada ya kifo cha Hayati Dkt.Magufuli.
"Pamoja na mafanikio makubwa ya rais Samia, wananchi wa wilaya ya Chato bado wanaendelea kumwomba atimize kiu yao ya kuwapatia mkoa hali itakayosaidia kuinua uchumi wa kaya,mkoa na taifa kwa ujumla" amesema Mch. Samson.
Mchungaji, Method Constantine, ameitaka jamii kuendelea kumwombea afya,hekima na busara,rais Samia ili aendelee kuwaongoza watanzania kwa amani na upendo hasa kuelekea kipindi cha uchaguzi wa serikali kuu hapo mwakani.
Amesema rais Samia amegeuka kuwa faraja kubwa kwa wananchi wa wilaya hiyo ambao baadhi yao walianza kukata tamaa kutokana na baadhi ya maneno ya watu waliokuwa hawaitakii mema wilaya hiyo kutokana na sababu zao binafsi.
"Kwa kweli tunayo matumaini makubwa sana na serikali yetu ya awamu ya sita,imefanya mambo mengi sana kwenye wilaya yetu,wakati Hayati Magufuli anafariki kuna miradi mingi ilikuwa haijakamilika lakini sasa mingi imekamilika tena kwa ubora na mingine inaendelea kujengwa"amesema Mch. Constantine.
Kwa upande wake, Mchungaji,Flora Innocent, amesema siri kubwa ya utulivu na amani ya nchi ni viongozi wa umma kushirikiana na viongozi wa dini katika mambo mbalimbali ya maendeleo pamoja na kupokea ushauri kutoka kwao.
"Maendeleo ya umma yanapatikana kutokana na ushirikiano mzuri wa viongozi wa dini na serikali,jamii inapokuwa na amani na utulivu hakika hata miradi mingi ya maendeleo inatekelezeka kwa ubora unaotakiwa"amesema Mch. Flora.
Mwisho.
Post a Comment