RAIS SAMIA ATANGAZA MSAMAHA KWA WAFUNGWA 1,548


............................

Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametangaza msamaha kwa Wafungwa 1548 ambapo Wafungwa 22 kati yao wameachiliwa huru leo December 09, 2024, na Wafungwa 1526 wanabaki gerezani kumalizia sehemu ya kifungo kilichobaki baada ya kupewa msamaha huu.

Taarifa iliyotolewa leo na Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema msamaha huo wa Rais Samia ni sehemu ya kuadhimisha Miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Rais ametumia Mamlaka aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1)(a) - (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kutoa msamaha huo huku akisema ni matarajio ya Serikali kuwa wafungwa hao watarejea tena katika jamii kushirikiana na wananchi wenzao katika ujenzi wa Taifa letu na kwamba watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani.

Imesema wafungwa wenye sifa mbalimbali wamepunguziwa robo ya adhabu zao wanazozitumikia hivi sasa baada ya punguzo la kawaida la moja ya tatu linalotolewa chini ya kifungu cha 49(1) cha Sheria ya Magereza sura ya 58.

Aidha imesema msamaha huo haukuwahusisha wafungwa wanaotumikia vifungo vya nje na wale waliowahi kukiuka masharti chini ya sheria ya Bodi ya Parole sura ya 400 (R.E 2002)

0/Post a Comment/Comments