Mkuu wa wilaya ya Chato,Louis Bura,akichimba msingi wa vyumba vya madarasa
...............
Na Daniel Limbe, Chato
WANANCHI wa kijiji cha Mwangaza kata ya Kasenga wilayani Chato mkoani Geita,wameiomba serikali kuwaboresha huduma ya elimu,afya,maji na miundombinu ya barabara huku wakidai wapo tayari kuendelea kuchangia miradi ya maendeleo itakayoelekezwa kwao.
Wamesema hayo baada ya mkuu wa wilaya ya Chato, Louis Bura, kuzindua rasmi mradi mpya wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa,Ofisi ya walimu na vyoo matundu sita kwenye shule ya msingi Mwangaza,mradi uliofadhiliwa na mfuko wa kunusuru kaya maskini nchini(Tasaf).
Mbali na uzinduzi huo wananchi wameonyesha kuguswa na mpango huo baada ya kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye kuchimba msingi,kukusanya mchanga, kokoto pamoja na maji ikiwa ni kutimiza takwa la aslimia 10 zinazopaswa kuchangiwa na jamii.
Kutokana na hali hiyo,mkuu huyo wa wilaya amelazimika kujumuika na wananchi hao kuchimba msingi wa vyumba vya madarasa huku akiwaomba wasimamizi wa mfuko wa Tasaf kuendelea kufadhili miradi mingine kwenye kata hiyo kutokana na mwitikio wa wananchi kushirikiana na serikali kuharakisha maendeleo.
"Naomba kukiri wazi kuwa katika ziara yangu iliyoanza tangu jana,ninyi hapa kijiji cha Mwangaza kata ya Kasenga mmefunika kote nilipopita,mmejitokeza wengi na mmeshiriki kikamilifu kutimiza mchango wenu wa aslimia 10, nitumie fursa hii kuwaomba Tasaf kama kuna mradi mwingine wowote wananchi hawa wapewe kipaumbele kwa sababu wana nia ya kupata maendeleo"amesema Bura.
Katika hatua nyingine,mkuu huyo wa wilaya amepongeza ushiriki wa wananchi kutoka kaya maskini kushirikishwa kikamilifu kwenye ujenzi wa barabara ya kijiji cha Ihanga yenye urefu wa km 4.1 iliyolimwa kwa kiwango cha vumbi na walengwa kulipwa fedha kutoka Tasaf.
Hata hivyo baadhi ya walengwa hao wameishukuru serikali kuendelea kuwaondolea umaskini wa vipato na kwamba angalau wameboresha maisha yao ukilinganisha na awali kabla ya kuanza kuhudumiwa na mfuko huo.
Vilevile baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mwangaza,wamesema ujenzi wa vyumba vya madarasa kwenye kijiji chao utasaidia kuondoa adha ya muda mrefu ya wanafunzi kusomea nje kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.
"Kwa kweli tunaishukuru sana serikali yetu kwa kuona umuhimu wa kuleta mradi huu mzuri kwetu,kama unavyoona shule hiyo imeanzishwa mwaka 1974 lakini mpaka leo baadhi ya watoto wanasomea chini kutokana na uhaba wa madarasa,mengine yamebomoka kama unavyoona" amesema Asteria Mathias.
Hata hivyo,kaimu mratibu wa Tasaf wilaya ya Chato,Isaya Kimwagile, amesema mbali na nguvu za wananchi wa mwangaza ujenzi wa vyumba hivyo,ofisi pamoja na matundu ya vyoo utagharimu kiasi cha shilingi milioni 74,498,089.
Amesema fedha zote zimekwisha pokelewa na halmashauri ya wilaya hiyo kutoka mfuko wa kunusuru kaya maskini nchini(Tasaf) na kwamba utekelezaji wake ndiyo umezinduliwa leo kwa lengo la kuhakikisha wananchi wananufaika na serikali yao.
Mbali na miradi hiyo,Bura ametembelea ujenzi wa zahanati ya Igando, ujenzi wa nyumba ya watumishi pamoja na kusikiliza kero za wanufaika wa mpango wa Tasaf kwenye kijiji cha Ihanga kata ya Buziku wilayani hapa.
Hakika ili jambo kubwa na jema lifanikiwe ni muhimu kulipokea kwa moyo wa upendo na dhati kama maneno ya mwana falsafa Alex Morrison aliyewahi kusema "Lazima uone kitu kizuri akilini kabla ya kukifanya".
Mwisho.
Post a Comment