*******
Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam
09/12/2024 Watu 182 wamepata huduma za kibingwa za uchunguzi
na matibabu ya moyo katika kambi maalumu ya upimaji iliyofanyika katika Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group ikiwa ni maadhimisho ya
miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika.
Upimaji huo umefanyika leo bila malipo yoyote yale katika
hospitali hiyo iliyopo TAZARA jijini Dar es Salaam ambapo watu wazima waliopata
huduma walikuwa 147 na watoto 35.
Akizungumza kuhusu upimaji huo Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Dkt. Tulizo Shemu alisema
kati ya watu wazima 147 walioonwa 72 walikutwa na matatizo mbalimbali ya moyo
ikiwemo shinikizo la juu la damu, matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo na
kutanuka kwa kuta za moyo.
Dkt. Shemu alisema watoto walioonwa walikuwa 35 kati ya hao
watano walikuwa na matatizo ya matundu kwenye moyo na mishipa ya damu ya moyo
kutokukaa katika mpangilio wake.
“Wananchi waliofika hapa wamepata huduma za kupima uwiano
baina ya urefu na uzito, wingi wa sukari kwenye damu, shinikizo la damu, mfumo
wa umeme wa moyo, jinsi moyo unavyofanya kazi, wamepata ushauri wa lishe bora
na wale waliokutwa na matatizo tumewapa dawa za kwenda kutumia”.
“Kupitia kambi hii
maalumu ya tiba mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuadhimisha siku
ya Uhuru wa Tanganyika kama rais wetu alivyosema iwe ni siku ya kufanya
shughuli za kawaida na kulinda afya nasi tukaona kulitekeleza hilo kwa
vitendo kwa kutoa huduma kwa wananchi
bila gharama zozote zile”, alisema Dkt. Shemu.
Dkt. Shemu ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo
alisema kupitia kambi hiyo mwitikio umekuwa mkubwa kwani sasa hivi jamii
inafahamu umuhimu wa kuchunguza afya zao pamoja na kuishi maisha ambayo
yatawawezesha kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi waliofika katika
kambi hiyo wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa kutoa fursa za uchunguzi wa afya kwa wananchi wa Tanzania.
Alex Kahela mkazi wa Arusha alisema alipata bahati ya
kuudhuria kliniki ya moyo iliyofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul
Makonda na kukutwa na tatizo la shinikizo la juu la damu aambapo wataalamu
walimpatia dawa na kushauriwa kuendelea kufanya uchunguzi wa mara kwa mara.
Kahela alisema baada ya kumaliza dawa zile aliamua kufika
Dar es Salaam kwaajili ya kufuatilia hali yake na kabla hajafika JKCI akakutana
na kambi hiyo ya siku ya Uhuru hivyo kubahatika tena kwa mara ya pili kufanyiwa
uchunguzi pamoja na kupata dawa bila gharama.
“Kwakweli namshukuru sana rais wangu kuwezesha kambi hizi za
matibabu kwani zinatusaidia sisi watu wa hali ya chini kupata huduma. Nakumbuka
kule Arusha nilikutwa na shinikizo la damu la 300 kwa 150, nilikuwa najisikia
vibaya lakini kwasababu sikuwa na uwezo wa kwenda hospitali nilikuwa naishi tu
hivyo hivyo”, alisema Kahela.
Kahela aliwaomba wataalamu wa afya wa JKCI kuendelea
kuwafikia wananchi wa hali ya chini ili nao waweze kupata huduma kwa wakati
kwani kwa hali aliyokuwa nayo Arusha kama asingepata matibabu labla leo
asingekuwa hai.
Naye Mariam Lema mkazi wa Dar es Salaam alisema amewahi
kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo huko nyuma lakini baada yakusikia JKCI
inatumia siku ya Uhuru kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo akaona naye atumie
fursa hiyo kupima kutokana na umri wake kuwa mkubwa.
Mariam alisema hivi sasa maradhi yamekuwa mengi hivyo ni muhimu kwa jamii
kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili pale changamoto inapojitokeza iwe
rahisi kutibika ikiwa ni katika hatua za mapema.
Mariam amewaomba wataalamu wa afya kuendelea kutoa elimu kwa
wananchi ya kuondoa hofu ili waweze kuzitumia kambi za matibabu ya magonjwa mbalimbali kufanya uchunguzi wa
afya na kupokea majibu yao bila ya kuwa na hofu.
“Watu wengi wamekuwa na hofu ya kufanya uchunguzi wa afya
kwamba wakikutwa na magonjwa haya makubwa maisha yao yatakuwaje na hivyo
kugundulika wakiwa katika hali mbaya inayopelekea usugu na wakati mwingine
kupoteza maisha”, alisema Mariam.
Post a Comment