DC CHATO: WANANCHI CHUKUENI TAHADHALI UGONJWA WA MARBURG


 Mkuu wa wilaya ya Chato,Louis Bura,akizungumza na waandishi wa habari

*******

Na Daniel Limbe,Chato

SIKU chache baada ya serikali kuthibitisha uwepo wa ugonjwa wa "Marburg" uliosababisha kifo cha mtu mmoja mkoani Kagera, serikali wilayani Chato mkoani Geita imewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhali ya ugonjwa huo kwa kuepuka safari zisizokuwa za lazima kuelekea mkoani Kagera.

Mbali na hilo,wametakiwa kuendeleza utamaduni wa kunawa na kutumia vitakasa mikono,kuepuka mikusanyiko, kusalimiana kwa kushikana mikono,kuepuka kushika mizoga ya wanyama,maiti na ambazo zimetokea katika mazingira ya kutatanisha.

Tahadhali hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya ya Chato,Louis Bura,wakati akizungumza na vyombo vya habari huku akisisitiza wananchi kutokuwa na taharuki badala yake waendelee kufanya kazi zao kama kawaida huku wakizingatia tahadhali zinazotolewa na wataalamu wa afya.

Amesema mpaka kufikia Januari 24,2025 wilaya hiyo bado haijapokea taarifa yoyote ya mshukiwa wa ugonjwa wa Marburg na kwamba hali hiyo haiwezi kuwa sababu ya kubweteka kwa kuwa wilaya ya Biharamulo na Chato ni majirani na wananchi wake wanatembeleana wakati wote.

"Nitumie fursa hii kuwasihi wananchi waendelee na kazi zao kama kawaida ispokuwa wachukue tahadhali tunazozitoa ili wilaya yetu iendelee kuwa salama" amesema Bura.

Akizungumzia mkakati wa halmashauri hiyo, Mganga mkuu wa wilaya Dkt. Aristides Raphael, amesema elimu ya afya inaendelea kutolewa kwa jamii hasa kwenye kata zinazopakana na wilaya ya Biharamulo na Muleba mkoani Kagera ili kuweka udhibiti wa haraka iwapo kutatokea mhisiwa wa ugonjwa huo.

Amezitaka kata hizo kuwa ni Bwongera,Nyarutembo,Kasenga na Katende huku akieleza kuwa baadhi ya zahanati,vituo vya afya pamoja na hospitali ya wilaya hiyo vimewekewa kitengo maalumu cha kupokea wahisiwa wa Marburg iwapo watapatikana.

Amezitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni,homa kali hasa nyakati za jioni,kichwa kuuma sana,tumbo,kikohozi,kuhara, kutapika na kutokwa na damu maeneo yote ya wazi yaliyopo kwenye mwili wa Binadamu.

Kadhalika amewataka wananchi kutoa taarifa haraka iwapo mtu atabainika kuwa na dalili zinazoshabihiana na ugonjwa huo ili wataalamu wa afya wachukue hatua za haraka kabla ya madhara makubwa kutokea.


                           Mwisho.

0/Post a Comment/Comments