BAJETI YA CHATO KUTATUA ADHA YA MABOMA YALIYO KWAMA


 ******

Na Daniel Limbe,Chato

BARAZA la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Chato mkoani Geita limepitisha makadilio ya bajeti ya shilingi bilioni 66,065,556,560 kwa ajili ya uendeshaji wa halmashauri hiyo,ikiwa ni pamoja na ukamilishaji wa maboma ya zahanati, vituo vya afya,shule za msingi na sekondari.

Hatua hiyo inakusudiwa punguza adha ya kutokamilika baadhi ya miradi iliyoanzishwa na wananchi na serikali kutakiwa kumalizia ujenzi wake.

Katika Baraza hilo ambalo kwa kauli moja limekubaliana kupitisha bajeti hiyo,lilijikita zaidi katika kuongeza nguvu za ukusanyaji wa mapato ya ndani na usimamizi bora wa miradi ya maendeleo.

Hata hivyo,Diwani wa Kata ya Ilyamchele,Phares Luhangija,mbali na kuipongeza halmashauri hiyo kwa kazi kubwa iliyofanyika katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2024/25 ameitaka kuongeza bidii katika ukamilishaji wa miradi iliyoanzishwa na wananchi badala ya kuanza mipya huku ya zamani ikiwa bado haijamalizika.

Kadhalika ameitaka halmashauri kutumia sheria zilizopo katika ukusanyaji mapato ili kuwabana wote wanaotorosha mapato ya serikali kinyume cha sheria.

Kwa upande Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Christian Manunga, ameagiza kutekelezwa kwa vitendo miradi yote iliyopewa fedha hatua itakayosaidia kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi.

"Pamoja na kupitisha makadilio ya bajeti mpya ya 2025/26 nikuombe mkurugenzi uendelee kusimamia utekelezaji wa fedha za miradi yote ambazo fedha zake bado zipo kwenye baadhi ya idara za halmashauri yetu ili zitumike kwa usahihi"amesema Manunga.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo,Mandia Kihiyo,amesema mpango huo wa bajeti unakusudia kuharakisha maendeleo ya wananchi wa wilaya ya Chato ikiwa ni pamoja na ujenzi wa majosho 15 katika mpango wa kunusuru kaya masikini nchini (TASAF) pamoja na kuimarisha mikopo ya aslimia 10 kwaajili ya wanawake,vijana na wenye ulemavu.

0/Post a Comment/Comments