Kuna Mtanzania mwenzetu anaitwa Juma Ally Maganga
ambaye ni dereva wa magari makubwa, inadaiwa anashikiliwa na Watu ambao wanadai
wao ni Askari Polisi Nchini Sudan Kusini, sababu ya kumshika ni kwamba
wanamtuhumua amemgonga mtu na kusababisha kifo wakati alipokuwa katika safari
zake akipita nchini humo.
Vyanzo vya taarifa zinaeleza kuwa bosi wa Mtanzania huyo anaitwa Gabriel John
Kiliki ni bosi wa Kampuni inaitwa Kiliki Company.
Juma akiwa anaendesha gari lenye namba za usajili T 931 CWS alisafiri kwenda
Sudan Kusini eneo la Juba ambapo ndipo ajali ilitokea, akapalekwa Kituo cha
Polisi cha Nimule.
Baadaye akahamishwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Malikia Police Station.
Siku ya tukio la ajali ilikuwa Februari 14, 2025, baada ya kushikiliwa, akapewa
nafasi ya kutoa taarifa kwa ndugu zake ambapo inadaiwa Polisi waliomshikilia
walianza kutoa maelekezo kuwa watumiwe fedha.
JamiiForums imewasiliana na mmiliki wa gari
alilokuwa akiendesha Juma Ally Maganga, mke wa dereva huyo na pamoja na upande
wa Wizara ya Mambo ya Nje
Mmiliki wa gari, Gabriel John Kiliki
Ni kweli dereva wangu Juma Ally Maganga ameshikiliwa tangu Februari 14, 2025,
tumeshatuma hela zaidi ya Tsh. Milioni 1 kwa Askari waliomshikilia ili
wamuachie lakini mpaka sasa bado kashikiliwa.
Kila tunapowasiliana na hao Askari Polisi wa huko wanakuwa wanataka hela lakini
hawakamilishi tunachokubaliana, baadaye wakataka tuwatumie Dola 3,500 ambazo
lakini hatujatuma mpaka sasa.
Pia, tunaendelea kuwasiliana na Mwenyekiti wa Madereva wa Malori wa Afrika
Mashariki anaitwa Sudi, anasaidia kuwasiliana na Polisi wa hapo.
Wakati huohuo, kuna madereva wangu wengine wa nne ambao nao wapo huko
wanashughulikia, gari pia alilopata nalo hiyo ajali wamelizuia mpaka sasa na
nimejulishwa dereva wangu huyo hali yake kiafya siyo nzuri kwa kuwa anaumwa,
alipigwa sana na Wananchi baada ya tukio kutokea.
Mke wa dereva, Rehema Godfrey Mongi
Wakati mume wangu anasafiri alikuwa na msaidizi wake ambaye ni mtoto wangu pia,
anaitwa Hassan Juma Maganga, baada ya tukio waliwapiga sana, walipofika Polisi
wakawapeleka kwenye kituo cha Afya baadaye wakawapeleka gerezani.
Walimuachia mwanangu ili apate nafasi ya kutoa taarifa kwetu, wamekuwa wakitaka
hela huko, tunatuma lakini hawamtoi.
Hela inapotumwa mwanangu akienda Kituo cha Polisi waliposhikiliwa awali,
wanaambiwa Askari aliyepokea fedha hayupo, mara hayupo zamu mara kaenda likizo.
Lakini pia kuna utata juu ya tukio hilo kwa kuwa wao wanasema ajali ilimhusisha
Mwanaume lakini kwenye taarifa ya Polisi inadaiwa wameandika aliyekufa ni
Mwanamke.
Tunaomba msaada Serikali itusaidie kumuokoa Mtanzania mwenzetu, nimeambiwa ana
kidonda kikubwa, anaumwa sana lakini bado wamemuweka ndani.
WIZARA YA MAMBO YA NJE
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mindi
Kasiga anasema "Nimewasilisha taarifa hii Idara ya Afrika leo asubuhi
(Februari 20, 2025) tulipoipokea. Wanafuatilia kwenye ofisi zetu za Ubalozi.
Naomba nikupe majibu pindi nitakapoyapata. Nashukuru kwa ushirikiano
wako."
Chanzo:Jamiiforums
Post a Comment