*********
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeipongeza Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yake, hususani miradi ya elimu inayotekelezwa Zanzibar. Pongezi hizo zimetolewa kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na TEA katika kuboresha miundombinu ya elimu na kuongeza fursa za ujifunzaji na ufundishaji katika ngazi zote za elimu.
Awali katika taarifa iliyowasilishwa mbele ya Kamati leo Februari 19, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Dkt. Erasmus Kipesha ilibainisha kuwa, ndani ya kipindi cha miaka mitano (2019/2020 – 2024/2025), TEA imetekeleza miradi mbalimbali yenye thamani ya takribani Shilingi Bilioni 2.8. Kati ya kiasi hicho, Shilingi Bilioni 2.1 zimetumika kuboresha miundombinu ya elimu, huku Shilingi Milioni 574.3 zikielekezwa katika kufadhili Mafunzo ya Kuendeleza Ujuzi (SDF) kwa vijana 600 kutoka kaya maskini.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Florent Kyombo alitoa pongezi hizo kwa niaba ya Kamati wakati wa ziara ya kikazi kisiwani Unguja Zanzibar, Februari 19, 2025. Ziara hiyo ililenga kukagua na kutathmini maendeleo ya miradi ya elimu inayotekelezwa na TEA pamoja na kupokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli za muungano katika sekta ya elimu.
Mhe. Kyombo alisisitiza kuwa TEA imefanya kazi kubwa katika kuboresha miundombinu ya elimu, na miradi yake imekuwa na manufaa makubwa kwa jamii. Alibainisha kuwa hata jimboni kwake, TEA imetekeleza miradi kadhaa kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa, hali inayoonyesha mchango mkubwa wa TEA katika kuinua ubora wa elimu nchini.
"Mamlaka
ya Elimu Tanzania inafanya kazi kubwa sana kwenye uboreshaji wa miundombinu ya
elimu kote nchini, siyo Zanzibar pekee. Ukipita maeneo ya vijijini na pembezoni
mwa miji, utaiona miradi yao mingi ambayo inaendelea kutatua changamoto za
miundombinu ya elimu," alisema Mhe. Kyombo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TEA, Dkt. Leonard Akwilapo, aliishukuru Kamati ya Bunge kwa kutambua juhudi za Mamlaka hiyo na kuahidi kuendelea kusimamia kwa weledi utekelezaji wa miradi yote ya elimu Tanzania Bara na Zanzibar. Pia alisisitiza kuwa TEA itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutafuta rasilimali kifedha ili kufadhili miradi mingi zaidi kwa maendeleo ya sekta ya elimu hapa nchini.
3. Mwenyekiti wa Bodi ya TEA, Dkt. Leonard Akwilapo (kushoto), akifuatilia taarifa ya utekelezaji wa majukumu na miradi ya elimu upande wa Zanzibar iliyowasilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania, Dkt. Erasmus Kipesha, mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria.
4. Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba naSheria wakisikiliza na kufuatilia taarifa ya utekelezaji wa majukumu na miradi ya elimu upande wa Zanzibar kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania, Dkt. Erasmus Kipesha.

6.
Post a Comment