TAMASHA LA MAJIMAJI LITUMIKE KULINDA RASILIMALI ZA NCHI-JENERALI MKUNDA



**************

Na Saidi Lufune – Ruvuma

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Jacob John Mkunda amesema maadhimisho ya miaka 120 ya kumbukizi ya Siku ya Mashujaa ya Vita vya Majimaji yanapaswa kutumika kama kielezo na somo tosha la ulinzi wa rasilimali za taifa zilizopo hapa nchini.

 Jenerali Mkunda amesema hayo  Februari 27, 2025 Mkoani Ruvuma akifunga tamasha la kumbukizi la vita vya Majimaji vilivyoanzia kusini mwa Tangangika mnano mwaka 1905 hadi 1907 ambapo amesema roho za mashujaa hao zitaendelea kuwa mbegu kutokana na moyo na uzalendo wa kulipigania Taifa lao.

“Watu hawa hawakua majambazi wala wavamizi bali ni watu waliojitolea kuulinda uhuru wao, utamaduni wao, heshima yao na rasilimali zao huku wakijua fika silaha zao zikiwa duni kuliko za wavamizi, lakini moyo wao wakizalendo uliwapa nguvu ya kusimama kwa pamoja na kupinga ukoloni hadi tone la mwisho” Amefafanua, Jenarali Mkunda

Aidha,  amewataka wananchi kujiepusha na uvivu, ubadhilifu wa mali za umma, matumizi ya dawa za kulevya na rushwa kwa kuwa kufanya hivyo ni kusaliti roho za mashujaa wa taifa hili na badala yake kutumia fursa zilizopo katika kufanya kazi kwa bidii ili kujipatia kipato na kuchangia ukuaji wa uchumi na pato la taifa 

‘‘Nitumie fursa hii kuipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa msukumo wa pekee kwenye sekta ya utalii nchini na kuufanya uchumi wetu kukua kwa asilimia 24.3 hadi kufikia mwaka 2023 na kuchangia kukua kwa pato la ndani kwa asilimia 17.2 kupitia sekta ya utalii’’. Amesema

Katika hatua nyingine Jenerali Mkunda amempongeza Waziri wa maliasili na Utalii  Mhe. Balozi. Dkt. Pindi Chana kwa kuitangaza vyema sera ya utalii ndani na nje ya nchi 

Ameutaka uongozi wa Mkoa wa Ruvuma kuunga mkono juhudi hizo kwa kufanya utafiti wa kubaini vivutio vipya vya Urithi wa Makumbo na Malikale ili kuongeza chachu katika ukuaji wa uchumi.

Akiongea kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Mkurugenzi Msaidizi wa Malikale na Makumbusho kutoka Wizara  hiyo Bw. William Mwita amesema kuwa pamoja na kuadhimishwa kwa kumbukizi za mashujaa hao Wizara inaendelea na mikakati ya ya kuhifadhi wa makumbusho ya Majimaji kwa kushirikiana na wadau katika kubaini maeneo yaliyotumika wakati wa vita vya Majimaji na kuyatangaza  kuingia katika orodha ya urithi wa Taifa. 


“Lengo ni kuhakikisha kuwa historia hii haishii tu kuwa kumbukumbu ya Taifa, bali pia inakuwa chachu ya utalii wa utamaduni, unaochangia katika maendeleo ya jamii na pato la jamii za mikoa ya kusini mwa Tanzania na Taifa kwa ujumla.”  Amesema Mwita


Mwita amesisitiza kuwa Wizara hiyo inaendelea na jitihada za kukusanya na kuhifadhi mikusanyo inayohusiana na vita ya Majimaji na kuyahifadhi Makumbusho ya Majimaji katika mkoa hua ili kutumika kama sehemu ya kujifunza, utafiti na vivutio kwa watajii kutoka ndani na nje ya nchi.

0/Post a Comment/Comments