***
Na Ester Maile_ Dodoma
Tangu Serikali ya Awamu ya Sita iingie madarakani, hali ya utendaji wa Bandari imeimarika ikiwemo kuongezeka kwa shehena mbalimbali ikiwemo shehena ya makasha, shehena ya nchi jirani pamoja na ongezeko la mapato.
Haya ya meelezwa na Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Plasduce Mbossa
Wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 24, 2025 jijini Dodoma
Ameeleza kuwa, katika kipindi hicho jumla ya shehena iliyohudumiwa na TPA imekuwa ikiongezeka kwa wastani wa asilimia 15.23 kwa mwaka kutoka tani milioni 20.78 mwaka wa fedha 2021/22 hadi tani milioni 27.55 mwaka wa fedha 2023/2024. Aidha, jumla ya shehena iliyohudumiwa katika bandari ya Dar es Salaam iliongezeka kwa wastani wa asilimia 13.38 kwa mwaka kutoka tani milioni 18.67 mwaka wa fedha 2021/22 hadi tani milioni 23.98 mwaka wa fedha 2023/2024.
“Katika kipindi cha miezi sita ya mwaka wa fedha 2024/25 (Julai-Desemba, 2024), jumla ya shehena iliyohudumiwa na bandari za TPA ni tani milioni 15.49 ambayo imezidi lengo lililowekwa la kuhudumia tani milioni 14.60 kwa asilimia 6.1 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 11.1 ikilinganishwa na tani milioni 13.94 iliyohudumiwa kipindi kama hicho mwaka uliopita”, amesema Mbossa.
"Ongezeko hilo limetokana na maboresho ya uendeshaji wa vitengo vya makasha vya bandari ya Dar es Salaam kwa kuviweka chini ya uendeshaji wa sekta binafsi wa Kampuni ya DP World Dar es Salaam na Tanzania East Africa Gateway Terminal Limited (TEAGTL)", amesema Mbossa.
Akizungumzia kuhusu kuongezeka kwa mapato ya TPA, yameongezeka kutoka shilingi trilioni 1.1 mwaka wa fedha 2021/22 hadi shilingi trilioni 1.475 mwaka wa fedha 2023/24 ambapo ongezeko hilo limetokana na mapato ya matumizi ya bandari, mapato ya kuhudumia meli pamoja na mapato ya mrabaha kwa tani au kasha linalohudumiwa na Kampuni ya DPW Dar es Salaam na Tanzania East Africa Gateway Terminal Limited pamoja na tozo la pango la maeneo ya bandari iliyolipwa na kampuni hizo kwenda serikalini kupitia TPA.
Kwa sasa TPA inasimamia bandari rasmi 131 zilizoko katika mwambao wa bahari ya Hindi na maziwa makuu ambapo katika mwambao wa bahari ya Hindi kuna bandari 32 na katika maziwa makuu kuna bandari 99.
Post a Comment