BARAZA LARIDHIA KUANZISHWA JIMBO JIPYA LA NYAKANAZI

Katikati ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo, Leo Rushahu,Kushoto ni makamu mwenyekiti, Erick Methord na kulia ni Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Innocent Mkandala.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Biharamulo, Innocent Mkandala.
Madiwani wakiwa katika mijadala
.............,..

Na Daniel Limbe, Biharamulo 

KIKAO cha Baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera,kwa kauli moja kimeridhia kugawanywa kwa Jimbo la Biharamulo magharibi ili kuanzishwa Jimbo jipya la Uchaguzi la Nyakanazi.

Kadhalika wameridhia kubadili jina la Jimbo la Biharamulo magharibi na kuwa Jimbo la Biharamulo, huku baadhi yao wakisisitiza kuwa ndoto yao ya kuhamia mkoa mpya wa Chato iko pale pale.

Katika hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wake,Leo Rushahu, kimesema wilaya hiyo inapaswa kuwa na majimbo mawili ya Uchaguzi kutokana na kukidhi vigezo vilivyowekwa na Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi(INEC) ikiwa ni pamoja Jimbo linalotakiwa kugawanywa lazima liwe na idadi ya watu wasiopungua 400,000 vijijini na 600,000 mijini.

Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 wilaya ya Biharamulo ilikuwa na idadi ya wakazi 457,114 kati yao wanawake 233,021 sawa na aslimia 50.98 na wanaume 224,093 sawa na aslimia 49.02 huku idadi ya kaya ikiwa ni 87,733.

Aidha Jimbo la Biharamulo Magharibi lina ukubwa wa kilomita za mraba 5,627 kati ya eneo hilo,km za mraba 5,617 ni nchi kavu ambapo eneo la makazi ni km 734 sawa na aslimia 13,huku eneo la km 1100 linafaa kwa ajili ya kilimo na eneo lenye maji likiwa ni km 10 ukiachilia mbali eneo la km za mraba 3,783 ambalo ni Hifadhi za taifa na mapori ya akina.

Kutokana na hali hiyo, madiwani hao wamesema jimbo lao linakidhi vigezo vyote vinavyostahili kugawanywa ili kusogeze huduma kwa wananchi na kuongeza kipato chao kutokana na takwimu kuonyesha kuwa wananchi hao kipato chao kimepanda kutoka Sh. 420,000 kwa mwaka hadi kufikia Sh. 720,000.

Hatua hiyo imetajwa kuchagizwa na hamasa kubwa iliyofanywa na serikali kwa wananchi wa wilaya hiyo kulima mazao ya Mihogo, Pamba,Tumbaku, Kahawa,Migomba, na mpunga, sambamba na kukamilika kwa barabara nyingi za vijijini hali iliyosaidia wakulima kufikisha mazao yao sokoni.

Wamezitaja kata pendekezwa katika Jimbo jipya la Nyakanazi kuwa ni Nyantakara,Kaniha,Kalenge,Nyanza,Lusahunga na Nyakahura.

Kadhalika Jimbo la Biharamulo, linatarajiwa kubaki na kata ya Biharamulo mjini,Ruziba, Bisibo, Nyamahanga,Nyarubungo,Runazi,Kabindi,Nyamigogo,Nyabusozi,Nemba na Katahoka.

Hata hivyo baada ya majadiliano ya kina madiwani wote wamepitisha azimio hilo na kumuomba mkurugenzi wa halmashauri hiyo,Innocent Mkandala, kuendelea na mchakato wa vikao vinavyofuata kabla ya mapendekezo hayo kupelekwa kwenye kamati ya ushauri ya wilaya(DCC) na ile ya mkoa (RCC) kwaajili ya kujadili na kuwasilisha kwenye Tume huru ya taifa ya Uchaguzi.

Uamuzi huo umetokana na Tangazo la Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi(INEC) la February 26,2025.

 

0/Post a Comment/Comments