GAVANA: UTAFITI UNAONESHA WANAWAKE WANA MATUMIZI MADOGO YA HUDUMA RASMI ZA KIFEDHA

********

Benki Kuu ya Tanzania imeendesha mkutano na viongozi mbalimbali wa sekta ya fedha, hususan sekta ya kibenki, pamoja na wadau wa maendeleo. Katika mkutano huo, wamejadili masuala mbalimbali yatakayosaidia kuziba pengo la kijinsia katika Huduma Jumuishi za Fedha nchini.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa Habari leo tarehe 5 Machi, 2025, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba, amesema utafiti wa Finscope wa mwaka 2023, unaonesha kuwa wanawake hawajafikiwa na wana matumizi madogo ya huduma rasmi za kifedha.

Ameongeza kuwa mkutano huo utajadili fursa zilizopo na namna ya kutumia fursa hizo katika kuziba pengo lililopo kati ya wanaume na wanawake katika upatikanaji na utumiaji wa huduma za fedha nchini.

Aidha, amesisitiza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayoandaliwa kwa upande wa Tanzania Bara, zinatazamia kuwa na uwiano wa asilimia Hamsini (50) kwa Hamsini (50) kati ya wanawake na wanaume ifikapo 2033.

Naye, Mwenyekiti wa Umoja wa Mabenki, Bw. Theobald Sabi, amesisitiza kuwa mabenki yanaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuwafikia wanawake wengi na biashara zinazomilikiwa na kundi hilo ili kufikia lengo la uwiano wa asilimia Hamsini (50) kwa Hamsini (50) kati ya wanaume na wanawake ifikapo 2033.

Amesema hatua hizo ni pamoja na ubunifu unaofanywa na benki za biashara katika kutengeneza bidhaa na huduma za kibenki mahususi kwa ajili ya wanawake ili kuondoa madhila mbalimbali yanayowakumba ikiwemo ukosefu wa mikopo.

Kwa upande wake, Meneja wa Taasisi ya Fedha ya Kimataifa (IFC) kwa nchi za Tanzania, Rwanda na Uganda, Bi. Martine Valcin, amesema suala la ujumuishi wa kijinsia katika upatikanaji na utumiaji wa huduma rasmi za kifedha ni la kipaumbele kwa Benki ya Dunia kutokana na mchango wake katika kustawisha uchumi wa Tanzania na dunia kwa ujumla.

Naye, Kiongozi wa Mpango wa Kuwawezesha Wajasiriamali Wanawake (WE-FI), Bi. Wendy Teleki, ameeleza kuwa Makubaliano ya Mpango wa Kuwawezesha Wajasiriamali Wanawake (Women Entrepreneurs Finance Initiative Code) uliozinduliwa leo unalenga kuzikutanisha taasisi za fedha ili kuingia kwenye makubaliano ya kuwawezesha kifedha wajasiriamali wanawake.







 

0/Post a Comment/Comments