KAMISHNA MKUU WA TRA AHIMIZA ULIPAJI KODI WA HIARI


...........

Na Ester  Maile Dodoma 

Kamishna Mkuu wa Mamlaka
 ya Mapato Tanzania (TRA)  Yusuph Juma Mwenda amewataka watumishi wa Mamlaka hiyo kuendelea kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan ya kusimamia ulipaji kodi wa Hiari.

Akifungua kikao cha nne cha Baraza la kwanza la Wafanyakazi wa TRA leo tarehe 04.03.2025 jijini Dodoma Kamishna Mkuu Mwenda amesema tangu alipoingia madarakani Rais wa awamu ya Sita alikuja na maelekezo mahususi kwa TRA ya kutaka kusiwepo na mabavu katika kukusanya Kodi.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema mbali na hayo Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kutoa maelekezo ya kuhakikisha kila anayestahili kulipa kodi analipa na kuwachukulia hatua wale wanaojihusisha na ukwepaji wa Kodi kwa namna mbalimbali wachukuliwe hatua za kisheria.

 Kufuatia maelekezo hayo na miongozo inayotolewa wameweza kuongeza makusanyo ya kodi na kuvuka malengo waliyowekewa na Serikali kwa miezi Saba mfululizo na kuwataka watumishi wa TRA kuendelea kuzingatia maelekezo hayo ili waendelee kuvunja rekodi ya makusanyo.

Kamisha  Mwenda ametaja miongoni mwa mambo yaliyowawezesha kuvuka malengo kwa miezi Saba mfululizo kuwa ni pamoja na ulipaji wa Kodi wa Hiari unaohusisha utolewaji wa Elimu kwa Mlipakodi na ziara za Viongozi kuwafuata Walipakodi na kuwasikiliza hali ambayo imewezesha kutatuliwa papo kwa hapo kwa changamoto za Walipakodi.

“Pamoja na wenzangu ndani ya TRA wakiwemo mameneja wa mikoa tumekuwa na utaratibu wa kuwafuata Walipakodi na kuzungumza nao katika maeneo yao hii imetusaidia sana kutengeneza uhusiano wa karibu na Walipakodi, na Mimi binafsi nimepita mikoa yote na nimekutana na Walipakodi” amesema Kamishna Mkuu Mwenda.

Hata hivyo uhuru uliotolewa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa TRA kufanya kazi zao bila kuingiliwa unapaswa kutumiwa ipasavyo kwa watumishi kujituma na kuhakikisha mianya yote ya ukwepaji kodi inazibwa hali ambayo itaendelea kuimarisha makusanyo ya kodi na kuleta usawa katika kukusanya Kodi.

Mwisho Mwenda amesema mapambano dhidi ya wakwepa Kodi yanapaswa kuongezeka ili kutowaumiza walipakodi waaminifu ambao wamekuwa wakifanya kazi zao  sehemu  moja na wasiolipa kodi jambo ambalo linapunguza ushindani wa kibiashara .

0/Post a Comment/Comments