MWANDISHI NGULI AFRIKA, SHAKA SSALI AFARIKI DUNIA

*****

Mwanahabari mashuhuri wa Uganda, Shaka Ssali, ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 71.

 Taarifa zinaeleza kuwa Ssali alifariki dunia Alhamisi, Machi 27, 2025, huko Virginia, Marekani.

Ssali, maarufu kama "Kabale Kid," alizaliwa katika Wilaya ya Kabale, Uganda. Maisha yake ya awali yalikuwa ya changamoto, akiacha shule na hata kuwa mwanajeshi wa utotoni kabla ya kuhamia Marekani, ambako alisoma na kupata shahada ya uzamivu (PhD) katika mawasiliano ya tamaduni mbalimbali kutoka Chuo Kikuu cha California, Los Angeles (UCLA).

Mwezi Mei 2021, Ssali alistaafu kutoka Idhaa ya Sauti ya Amerika (VOA) baada ya kufanya kazi kwa miaka 29, ikiwa ni pamoja na zaidi ya miongo miwili kama mwanzilishi, mtangazaji, na mhariri mkuu wa kipindi cha Straight Talk Africa. Kipindi hicho kilitoa jukwaa muhimu kwa viongozi wa Afrika, wachambuzi, na wananchi kujadili masuala ya demokrasia, utawala, na maendeleo ya bara hilo.

Katika taaluma yake, Ssali alifanya mahojiano na viongozi wakuu wa Afrika, wakiwemo marais na mawaziri wakuu, huku akihakikisha sauti za wananchi wa kawaida zinajumuishwa katika mijadala kuhusu uongozi na maendeleo.


 

0/Post a Comment/Comments