Tume ya Ushindani Nchini (FCC) imezindua wiki ya Kitaifa ya siku ya kumlinda Mlaji Duniani ambayo hufanyika kila mwaka Marchi 15 ambapo katika wiki hiyo watajikita kutoa Elimu kwa Wananchi ili kuwa na uelewa kuhusu Haki za Mlaji na hivyo kushiriki kikamilifu katika kuchangia Maendeleo ya Taifa.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC) William Erio akizungumza na
Waandishi wa habari Jijini Dar es salaam wakati wa Uzinduzi huo amesema Haki za
Mlaji ni pamoja na Kuchagua, Kulinda, Kupata taarifa na Kusikiliza huku
akisisitiza Wadau kutumia kipindi hicho kutembelea Ofisi za FCC na kufuatilia
vipindi mbalimbali vitakavyokuwa vikirushwa kupitia vyombo vya habari.
Kwa kuadhimisha wiki hii, FCC imeandaa programu mbalimbali za utoaji elimu kwa
wadau kama vile wanafunzi wa vyuo vikuu, wafanyabiashara, na wananchi kwa
ujumla. Pia, kutakuwa na kliniki maalum kwa ajili ya kutoa msaada wa kisheria
kwa wateja wanaokumbana na changamoto katika soko.
FCC mwaka huu imechagua kaulimbiu inayolenga haki na maisha endelevu kwa mlaji,
huku ikihimiza matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kupunguza uchafuzi wa
mazingira na kuhakikisha mlaji anapata bidhaa bora zinazomlinda kiafya na
kimazingira.
Katika kuunga mkono Siku ya Wanawake Duniani, FCC imeandaa zoezi maalum la
upimaji wa saratani ya matiti na shingo ya kizazi kwa wanawake, kama sehemu ya
kuhakikisha ustawi wa jamii na afya bora kwa wote.
Aidha, Erio amewatakia heri waumini wa dini ya Kiislamu na Wakristo katika
mfungo wa Ramadhani na Kwaresima, huku akihimiza wananchi kutembelea ofisi za
FCC ili kupata elimu zaidi kuhusu haki zao kama walaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kudhibiti Mienendo ya Kibiashara Inayokatazwa na
Sheria ya Ushindani kutoka FCC, Magdalena Utou amesema kuwa lengo kuu la wiki
hii ni kuwajengea wananchi uelewa kuhusu haki na wajibu wao katika soko.
Pia, Meneja Miradi wa taasisi ya FCS, Charles Kainkwa, amesema taasisi yake
inashirikiana na FCC chini ya TradeMark Africa ili kuhakikisha elimu kuhusu
haki za mlaji inawafikia wananchi wengi zaidi, kuwajengea uwezo wa kufanya
maamuzi sahihi wanaponunua bidhaa na huduma.
Kauli mbiu ya siku hiyo ni Haki na Maisha endelevu kwa Mlaji
yenye lengo la kuhamasisha chaguzi zinazotunza Mazingira, Matumizi Bora ya
rasimali.
Post a Comment