Na Daniel Limbe,Chato
KUELEKEA kumbukizi ya miaka minne ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, Machi 17,2025, maelfu ya watanzania wamejitokeza kwenye matembezi ya amani kumuenzi kwa mambo makubwa aliyotekeleza enzi za uhai wake.
Mbali na matembezi hayo, familia ya Hayati Dkt. Magufuli imetoa zawadi mbalimbali kwa wagonjwa waliolazwa kwenye hospitali ya rufaa ya Kanda Chato (CRZH) ikiwa ni matendo ya huruma kwa wahitaji.
Katika matembezi hayo yenye umbali wa takribani km 3 yaliyo ratibiwa na familia kwa kushirikiana na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) yamewahusisha watu mbalimbali ikiwemo baadhi ya viongozi wa serikali,wafanyabiashara na wadau wengine wa maendeleo.
Wakiwa katika hospitali ya rufaa Kanda ya Chato, wamempongeza Hayati rais Magufuli kwa maono yake ya kuanzisha miradi mikubwa ya kitaifa ikiwemo ujenzi wa hosptali hiyo ambayo kwa sasa inahudumia wagonjwa zaidi ya 40,000 kwa mwaka.
Imeelezwa kuwa kabla ya uwepo wa hospitali hiyo,wananchi walikuwa wanalazimika kusafiri umbali mrefu kupata huduma za matibabu ya kibingwa na ubobevu kupitia hospitali ya Bugando Mwanza na Hospitali ya taifa Muhimbili.
Akizungumza kwa niaba ya familia ya Hayati Dkt. Magufuli,mtoto wa marehemu Jesca John Magufuli,amesema familia hiyo inaungana na watanzania wote kuelekea kumbukizi ya kifo cha mzazi wao kwa kutoa matendo ya huruma kwa wagonjwa wenye uhitaji.
Amempongeza rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake kubwa ambazo ameendelea kuzionyesha kwa watanzania ikiwa ni pamoja na kuendeleza mema yote yaliyoachwa na mtangulizi wake aliyekuwa rais wa awamu ya tano.
Kwa upande wake,mgeni rasmi katika matembezi hayo,Makamu mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Taifa( UVCCM), Rehema Sombi, amedai kuridhishwa na kazi kubwa iliyofanywa na Hayati rais Dkt. Magufuli, katika ujenzi wa hospitali hiyo ambayo imekuwa kimbilio la wagonjwa kutoka nchi za Kongo,Rwanda,Uganda na Burundi.
Kadhalika amempongeza rais Dkt. Samia kwa kuendelea kukamilisha miradi mikubwa iliyoachwa na mtangulizi wake na kwamba utekelezaji huo ni mafanikio makubwa ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM).
Awali Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya rufaa Kanda ya Chato,Dkt. Osward Lyapa,amesema uwepo wa huduma za kibingwa na bobezi kwenye hospitali hiyo umesaidia sana jamii kupata huduma bora na za uhakika katika maeneo yaliyo karibu yao ukilinganisha na awali walipokuwa wakilazimika kwenda Hospitali ya taifa Muhimbili.
Baadhi ya wagonjwa waliolazwa kwenye hospitali hiyo,mbali na kushukuru kwa msaada wa matendo ya huruma waliokabidhiwa kutoka familia ya Hayati Dkt. Magufuli, wamepongeza huduma bora zinazotolewa na wataalamu wa hospitali hiyo,ambapo baadhi ya waliojifungua wamewapatia watoto wao jina la John na Jesca Magufuli ikiwa ni kuenzi mchango mkubwa wa Hayati rais Magufuli.
Aidha kesho Machi 17,2025,Familia ya Hayati Dkt. Magufuli itaungana na Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge Ngara,kuadhimisha Misa maalumu ya kumbukizi ya miaka minne ya kifo cha mzazi wao, aliyekuwa rais wa Tanzania kabla ya kukumbwa na umauti wakati akipatiwa matibabu ya changamoto ya umeme wa moyo.
Makamu mwenyekiti UVCCM taifa, Rehema Sombi,akizungumza na wananchi wilayani Chato
Mwisho
Post a Comment