Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imeungana na Ubalozi wa
Uingereza pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa – Mpango wa Chakula Duniani
(World Food Programme - WFP) katika kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati
safi ya kupikia mashuleni.
Uhamasishaji huu ulifanyika kupitia warsha maalum iliyowakutanisha walimu
wakuu, wapishi, na walimu wa lishe kutoka shule 50 za Halmashauri ya Manispaa
ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Warsha hiyo iliyofanyika tarehe 27 Machi 2025, katika Shule
ya Msingi Liwati, ililenga shule zinazotarajiwa kufadhiliwa na WFP ili kuanza
kutumia nishati safi ya kupikia.
Katika warsha hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa
Miradi ya Elimu wa TEA, Bw. Masozi Nyirenda, aliambatana na Kaimu Meneja wa
Utafutaji Rasilimali na Hamasa wa TEA, Dkt. George Mofulu.
Nyirenda aliwaeleza wadau wa nishati safi ya kupikia kuwa
TEA iko mbioni kutafuta zaidi ya Shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kutekeleza
mradi wa kuwezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwenye takriban shule
500 za sekondari nchini ndani ya kipindi cha miaka mitano.
Aidha, alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wadau kushirikiana
na TEA kwa kufadhili mradi huo ili kutunza mazingira ya ujifunzaji na
ufundishaji.
Kwa upande mwingine, Balozi wa Uingereza nchini, Bi. Marianne Young pamoja na
Mwakilishi wa WFP nchini, Bw. Ronald Tran Ba Huy, walipongeza Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi zake za kuhamasisha matumizi ya
nishati safi ya kupikia mashuleni na wakaahidi kuendelea kuunga mkono juhudi
hizo.



Post a Comment