Ramani ya majimbo ya Chato kaskazini na Chato kusini.
................
Na Daniel Limbe,Torch media
SIKU moja baada ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kutangaza majimbo mapya nane ya likiwemo la Chato kusini, wananchi pamoja na viongozi mbalimbali wilayani Chato mkoani Geita wameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuandika historia mpya ya kupatikana Jimbo hilo.
Kwa mujibu taarifa iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Mahakama ya rufaa, Jacobs Mwambegele, ni rasmi wilaya ya Chato itakuwa na majimbo mawili ya Uchaguzi ambayo ni Chato kaskazini na Chato kusini.
Jaji Mwambegele alisema Tume hiyo ilipokea maombi 34 kutoka majimbo mbalimbali yaliyohitaji kugawanywa, lakini kutokana na vigezo vilivyowekwa pamoja na ukubwa wa jengo la Bunge ni majimbo nane pekee ndiyo yalikubaliwa na INEC ikiwemo Jimbo la Chato Kusini.
Hatua hiyo imeibua shangwe kwa baadhi ya wananchi na viongozi mbali mbali akiwemo Goodluck Phinias na Roza Micheal ambao wameishukuru INEC kwa kukubali kuligawa Jimbo hilo na kwamba uamuzi huo unakusudiwa kuchochea maendeleo ya Umma kwa haraka zaidi.
"Tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuandika historia mpya katika utawala wake kwa kupatikana Jimbo jipya la uchaguzi la Chato kusini,maana hii ilikuwa ni kiu kubwa ya wananchi,"
"Vile vile pongezi zingine tunazielekeza kwa Tume Huru ya Taifa Uchaguzi kwa kupitia vigezo mbalimbali hatimaye kukubali kuligawa Jimbo letu, nimatumaini yetu sasa Chato inakwenda kupiga hatua kubwa za kimaendeleo" amesema Phinias.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Chato, Louis Bura, amempongeza Rais Samia kwa hatua kubwa za kuwasogezea maendeleo wananchi na kwamba kupatikana kwa jimbo jipya itasaidia kutatua baadhi ya changamoto za maendeleo zilizokuwa zinakwama kutokana na bajeti ndogo kwa jimbo moja lililokuwepo awali.
Amesema uwepo wa wabunge wawili kwenye wilaya hiyo utasaidia wananchi kufikisha mahitaji yao kwa haraka zaidi Bungeni kupitia wawakilishi watakao wachagua.
"Kuelekea Uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani mwaka huu, niwasihi wananchi watumie fursa hiyo kuchagua wawakilishi wao ili tupate viongozi wazuri wenye moyo na maono ya kuwatumikia" amesema Bura.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Chato,Mandia Kihiyo,mbali na kumpongeza Rais Samia kwa uhiari wake kugawanywa majimbo mapya ya uchaguzi, amesema hatua hiyo itakwenda kuboresha miundombinu ya wananchi kupitia mifuko ya Jimbo na utatuzi wa changamoto zingine ambazo hupata fedha kupitia uwakilishi wa majimbo.
"Tunatarajia kutatua kero nyingi za wananchi kupitia mfuko wa barabara, maji pamoja na afya na kwamba wananchi wetu watafikiwa na uwakilishi kwa wepesi zaidi" amesema Kihiyo.
Aidha ameishukuru INEC kwa kukamilisha mchakato huo kwa amani na kwamba muda uliosalia ni kupokea maelekezo mengine kutoka Tume iwapo yatakuwepo ili kukamilisha taratibu za maandalizi ya uwakilishi kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Mbali na Kugawanywa kwa Jimbo la Chato kusini,majimbo mengine na mikoa yake kwenye mabano ni Katoro(Geita), Itwangi(Shinyanga) Bariadi mjini(Simiyu), Uyole(Mbeya),Mtumba(Dodoma),Kivule na Chamazi(Dar es salaam).
Ongezeko la majimbo hayo inafanya idadi ya majimbo nchini kutoka 264 hadi 272 huku Tanzania Bara ikiwa na majimbo 222 na Zanzibar 50.
Mwisho.
Post a Comment