Na Daniel Limbe,Torch media
WANANCHI wilayani Biharamulo mkoani Kagera wametakiwa kuheshimu mipaka ya maeneo yaliyotengwa kwaajili ya matumizi bora ya ardhi ili kuepusha migogoro isiyokuwa ya lazima katika jamii.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo,Innocent Mkandara,ametoa agizo hilo kwenye kikao cha Baraza la madiwani wa halmashauri hiyo na kuwataka watendaji wa Umma kusimamia kikamilifu agizo hilo.
Hatua hiyo imekuja baada ya Diwani wa kata ya Kabindi, Philbert Rubula, kuibua hoja ya uwepo wa migogoro ya wakulima na wafugaji kwenye kata yake huku akiiomba halmashauri hiyo kuwaongezea wananchi eneo kwaajili ya shughuli za ki binadamu.
Amesema licha ya kazi nzuri inayotekelezwa na halmashauri hiyo bado kwenye kata yake kuna taabu kubwa ya migogoro ya wakulima na wafugaji na kwamba hatua za haraka zisipo chukuliwa huenda ikasababisha madhara zaidi.
Licha ya Diwani huyo kuwasilisha hoja yake kwa hisia kali, bado msimamo wa mkurugenzi huyo haukuteteleka baada ya kuwataka wananchi kuheshimu mipaka iliyoainishwa kwaajili ya matumizi bora ya ardhi.
"Ninachoweza kusema ni kwamba jamii lazima iheshimu matumizi bora ya ardhi, maana ardhi ni ile ile japo watu na shughuli za kibinadamu zinaongezeka, pasipo kufanya hivyo migogoro itaendelea kwenye maeneo yenu,maana hakuna eneo la kumega ili kuwapa wananchi" amesema Mkandara.
Mbali na hilo, amewataka wananchi wa kata hiyo kulima mazao yanayo stahimili mvua chache badala ya kulima kwa mazoea jambo lililosababisha wakulima wengi kutopata mavuno mazuri ya maharage katika msimu huu.
Kadhalika amewasihi kufuatilia ushauri unaotolewa na Mamlaka ya hali ya hewa nchini(TMA) ili kuwa na kilimo chenye uhakika na mavuno yenye tija.
Post a Comment