WAFUGAJI ZINGATIENI SHERIA ILI KUMALIZA MIGOGORO NA WAKULIMA' ACP MPINA

:::::::


Afisa wa Polisi Jamii Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Lwele Mpina amewataka wafugaji kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za matumizi ya ardhi ili kumaliza migogoro ya mara kwa mara kati yao na wakulima.

Kamishna Mpina amebainisha hayo leo Mei 22,2025, katika Mtaa wa Mitimilefu, Kata ya Magu Mjini mkoani humo wakati akitoa elimu kwa wafugaji wa vijiji vya kata ya Magu mjini kufuatia kuongezeka kwa malalamiko ya mifugo kuharibu mashamba ya wakulima, jambo linaloibua migogoro inayohatarisha amani katika jamii.

“Kupeleka mifugo na kulisha kwenye mashamba ya wakulima siyo tu ni kuvunja sheria, bali ni kuchochea uhasama unaoweza kusababisha migogoro mikubwa acheni tabia hiyo, ” amesema Mpina.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Magu, Fundikila Fundikila amekiri kuwepo kwa migogoro midogo kati ya wakulima na wafugaji ambapo amesema Serikali imekuwa ikikutana na makundi hayo na kutoa elimu sambamba na kuwaelekeza sheria na taratibu wanazotakiwa kuzingatia katika mamlaka za miji.

"Tumekuwa tukiwahimiza wafugaji kupunguza idadi ya mifugo na kuwa na mifugo michache itakayoleta tija kwenye maisha yao, pia kupitia mikutano tumekuwa tukiwafundisha sheria mbalimbali zinazosimamia mifugo ikiwemo sheria ndogo ndogo za halmashauri" amesisitiza Fundikila

Wakiwasilisha kero mbalimbali wakati wa mkutano huo, baadhi ya wafugaji wameoneshwa kukerwa na baadhi ya tabia za wafugaji wenzao kwa kukosa hekima kwa wakulima pindi mifugo inapokula mazao shambani.
 
"Mchungaji wa ng'ombe akiwa anachunga akimuona mkulima anamsemesha yeye anaongeza sauti ya redio" Amesema Selilo Elisha 

Kwa upande wake, Hafaksad Lwambo (mfugaji) kutoka kata ya Isandula, wilayani humo amesema elimu waliyoipata itawasaidia kujiepusha na migogoro ya wakulima na wafugaji. Aidha, ameomba elimu hiyo iwe endelevu kwa makundi yote ili wote wapate uelewa wa pamoja.

Hata hivyo, Mkuu Polisi Wilaya ya Magu mkoani humo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Haji Makame ametoa onyo kali kwa wafugaji watakaokiuka maagizo haya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao, ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kuajiri watoto katika shughuli za kuchunga mifugo na kuchochea migogoro ya kijamii.



 

0/Post a Comment/Comments