Na Daniel Limbe,Torch media
WANAFUNZI wa kitongoji cha Iyozu kata ya Muungano wilayani Chato mkoani Geita wanalazimika kutumia mitumbwi kutoka kwenye makazi yao kwenda shuleni kutokana na mvua kubwa zilizonyesha miaka 13 iliyopita kukata mawasiliano ya kitongoji hicho kwenda kwenye kijiji cha Rubambangwe.
Inaelezwa kuwa wanafunzi hao wanasoma shule ya msingi Rubambangwe na wengine sekondari ya Rubambangwe katika kijiji hicho,ambapo baada ya kufanikiwa kuvuka maji hulazimika kutembea umbali wa zaidi ya km 4 ili kufika shule wanazosoma.
Pia hali hiyo imekuwa ikisababisha baadhi ya wanafunzi kuzama maji wakati wa kuvuka baada ya mitumbwi wanayosafiria kupinduka hivyo kutishia uhai wa maisha yao kutokana na eneo hilo kuwa na wanyama hatarishi kama mamba,nyoka na samaki aina ya Kamongo.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida mwandishi wetu amefanikiwa kufika eneo la tukio na kushuhudia wanafunzi wakivuka na mtumbwi pasipo kuwa na uangalizi wa mtu mzima yoyote,(Picha tumezihifadhi) huku baadhi yao wakipiga kasia ili kuhakikisha wanafika salama ng'ambo ya pili.
Kutokana na hali hiyo, wazazi,walezi na wakazi wa kitongoji hicho wameiomba serikali kuwajengea daraja la kuvuka kwa miguu ili kunusuru maisha ya watoto na wajawazito ambao baadhi yao wamekuwa wakijifungulia njiani kutokana na mazingira mabovu ya kufika kwenye huduma za afya.
"Tunaiomba serikali yetu kupitia kwa Rais wetu mpendwa Samia Suluhu Hassan,itusaidie wananchi wa Iyozu kwa kutujengea daraja ili kutuepusha na adha tunazopitia sisi na watoto wetu, maana mara kwa mara wanafunzi wamekuwa wakizama maji na kuokolewa katika hali mbaya,"
"Kilio chetu kimekuwa cha muda mrefu pasipo ufumbuzi wa kudumu,hatuna pa kukimbilia wakati huku ndiko kwenye makazi na maisha yetu, zaidi tunaiomba serikali isikilize kilio chetu ili kunusuru maisha ya wajawazito na wanafunzi wetu." amesema Barisimaki Maka.
Zuberi Mtani, mkazi wa Iyozu anasema juzi mei 11,2025 alifanikiwa kuwaokoa wanafunzi watatu waliozama maji wakati wakivuka na mtumbwi kwenda shule na kwamba kama pasingekuwa na watu wazima ndani ya usafiri huo watoto hao wangekumbwa na umauti kutokana na kina kirefu cha maji eneo hilo.
Akizungumza kwa niaba ya mwenyekiti wa kijiji cha Rubambangwe,mwenyekiti wa kitongoji cha Iyozu,Fallu Masasila, amekiri wanafunzi kutumia usafiri wa mitumbwi kuvuka kwenda shule na jioni kurejea nyumbani,adha iliyodumu kwa takribani miaka 13 pasipo kupatikana ufumbuzi wa kudumu.
Anasema watoto wanapo kwenda shule roho za wazazi wao hubaki na mashaka ya usalama wa maisha yao, huku Sikuamini Mabina pamoja na Abia Majura, wakiomba hatua za haraka na dharura kuchukuliwa kutatua changamoto hiyo kutokana na kitongoji hicho kuonekana kutengwa na miundombinu ya barabara ukilinganisha na maeneo mengine.
Diwani wa Kata ya Muungano, Charles Kapembe, amethibitisha uwepo wa changamoto hiyo na kudai kuwa tayali ameshawasilisha maoni ya wananchi hao kwenye vikao halali vya Baraza la madiwani pamoja na kuzungumza na moja kwa moja mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo kwaajili ya utatuzi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo,Mandia Kihiyo, amesema tayali amefanya ziara eneo hilo na kujionea hali ilivyo na kwamba halmashauri hiyo inakusudia kuchonga mtumbwi wenye thamani ya shilingi milioni mbili ili kupunguza adha ya wananchi kuvuka eneo hilo.
"Kwa hatua ya awali tunakusudia kutengeneza mtumbwi mzuri kwaajili ya kutoa huduma ya kuvukisha watoto na wananchi wengine,na kadili tutakavyo endelea kupata pesa tutajenga daraja eneo hilo na ndiyo itakuwa njia ya kudumu kwa kero kubwa iliyopo eneo hilo."amesema Kihiyo.
Barisimaki Maka,akizungumza na waandishi wa habari
Mwisho.
Post a Comment