:::::::
Rabat, Morocco
Serikali ya Uingereza imeunga mkono rasmi mpango wa Morocco wa kuipa Sahara mamlaka ya ndani (autonomy), ikisema kuwa huo ndio mpango wa kweli, wa kuaminika na unaotekelezeka zaidi katika kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro huo wa muda mrefu.
Msimamo huo umetolewa jijini Rabat, baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, David Lammy, kukutana na mwenyeji wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco, Nasser Bourita, ambapo walitia saini tamko la pamoja kuhusu uhusiano wa pande hizo mbili.
“Uingereza inauona Mpango wa Uautonomi wa Morocco kuwa ndio msingi wa kuaminika, wa kiuhalisia na unaotekelezeka zaidi katika kutatua mzozo wa Sahara,” imesema sehemu ya tamko hilo la pamoja.
Uingereza imetoa wito kwa pande zote zinazohusika kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kisiasa unaoongozwa na Umoja wa Mataifa. Serikali hiyo pia imesisitiza kuwa utatuzi wa mgogoro huo utaleta utulivu Afrika Kaskazini na kusaidia ushirikiano wa kikanda.
Katika hatua ya kuunga mkono maendeleo, Uingereza imetangaza kuwa taasisi yake ya UK Export Finance iko tayari kufadhili miradi ya maendeleo katika Sahara ya Morocco, kupitia mfuko wake wa pauni bilioni 5 kwa ajili ya miradi mbalimbali nchini humo.
Waziri Lammy alisema Morocco ni mshirika wa kimkakati wa Uingereza na lango muhimu kwa maendeleo ya Afrika, huku akieleza dhamira ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo.
Mpango wa Morocco pia unaungwa mkono na mataifa mengine kama Marekani, Hispania, Ufaransa na Kenya. Hili linaongeza nguvu kwa hoja ya kuwa mpango huo ndio suluhisho pekee la kweli kwa mgogoro wa Sahara Magharibi.
Aidha, Uingereza imerejea kuunga mkono juhudi za Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Staffan de Mistura, na imesisitiza haja ya kupata suluhu inayokubalika kwa pande zote kwa njia ya mazungumzo na maridhiano.
Kwa hatua hii, Uingereza imejiunga na jumuiya ya kimataifa inayoamini kuwa mpango wa Morocco ndio njia ya kuleta utulivu na maendeleo endelevu katika ukanda wa Maghreb na Afrika kwa ujumla.
Post a Comment