Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya uzinduzi wa kituo cha Biashara na usafirishaji Afrika Mashariki kilichojengwa eneo la Ubungo Jijini Dar es salaam August mosi mwaka huu ikiwa ni katika mpango wa Serikali ya Tanzania kuimarisha fursa za kibiashara na uwekezaji.
Akizungumza jijini Dar es salaam katika mkutano na waandishi wa habari Mkuu wa Mkoa huo Mhe Albert Chalamila amewataka wakazi wa Jiji hilo na watanzania kwa ujumla hususani waliokwisha chukua maeneo ya kufanyia biashara na wale wenye nia ya kufanya biashara kwenye kituo hicho kujitokeza kwenye uzinduzi huo ili kujionea uwekezaji uliofanywa na serikali ya awamu ya sita pamoja na kuona fursa za kibiashara zilizopo kwenye kituo hicho.
RC Chalamila amesema kuwa Serikali iliamua kuhamisha kituo cha mabasi ya mikoani na nje ya nchi kilichokuwa eneo la Ubungo na kukihamishia Mbezi ambapo imetumia zaidi ya dola za marekani milioni miamoja kujenga kituo hicho cha biashara na usafirishaji Afrika Mashariki chenye zaidi ya maduka 2000 hivyo kituo hicho kinazinduliwa rasmi Augost Mosi na Rais Dkt Samia ili lengo la ujenzi huo la kuongeza fursa za biashara liweze kutimia.
Sanjari na hayo RC Chalamila amesema kuwa kituo hicho kimejengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo na muwekezaji kutoka nchini China huku akisisitiza kuwa ushiriki wa wawekezaji kutoka China si kwa lengo la kupoka fursa za wawekezaji wazawa bali ni mfumo wa uwekezaji wenye manufaa makubwa kwa watanzania
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Albert Chalamila amewataka watanzania kutumia fursa ya uwepo wa mashindano ya mpira wa miguu ya CHAN kuweza kufanya biashara kwani Mkoa huo kupitia Idara ya biashara umeandaa maonesho ya wafanyabiashara wadogo na wakubwa kwenye eneo la kuzunguka uwanja wa mpira wa Benjamin Mkapa
Aidha RC Chalamila amewataka watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki uzinduzi wa CHAN August 2 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Mkoa tayari umeshandaa mabasi miamoja kwa kila Wilaya ili kuwezesha watanzania kufika uwanjani, pia amewataka bodaboda,bajaji na wamiliki wa hoteli waliopo jijini humo kitumia fursa ya ugeni huo kufanya biashara
Ifahamike kuwa uzinduzi wa kituo cha biashara Afrika mashariki pamoja na uwepo wa mashindano ya CHAN na baadae ACFCON ni fursa muhimu za kibiashara kwa watanzania
Post a Comment