Aibua maeneo ya uwekezaji, ushirikiano zaidi na Tanzania_
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefanya mazungumzo na Rais Mteule na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Biashara ya Afrika (Afreximbank), Dkt. George Elombi na kuainisha maeneo zaidi ya uwekezaji nchini Tanzania.
Mheshimiwa Majaliwa amesema anaamini kuwa katika kipindi cha uongozi wa Dkt. Elombi, benki hiyo itaongeza kwa kiwango kikubwa mchango wake katika kusukuma mbele biashara, maendeleo ya viwanda na uwekezaji wa kimkakati barani Afrika ikiwemo Tanzania.
“Tunapenda kukuhakikishia kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea kujitolea kikamilifu katika ushirikiano wake wa kimkakati na Afreximbank,” alisema.
Katika mazungumzo hayo, Mheshimiwa Majaliwa alihimiza umuhimu wa Afreximbank kukamilisha mpango wake wa ujenzi wa kituo cha kisasa cha tiba nchini Tanzania (African Medical Centre of Excellence) ambacho kitakuwa na uwezo wa kutoa huduma bora za afya kwa wananchi na pia kupunguza utegemezi wa rufaa za nje ya nchi kwa matibabu maalum.
Aidha, Waziri Mkuu aliitaka benki hiyo iendelee kuzingatia utekelezaji wa miradi ya kimkakati nchini Tanzania, akisisitiza kuwa Tanzania ina mazingira mazuri ya uwekezaji na miradi yenye tija katika sekta mbalimbali. “Usaidizi wa kifedha kutoka Afreximbank, utaongeza kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo na kuchochea maendeleo ya kiuchumi,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimweleza Rais Mteule umuhimu wa kuwekeza katika uchumi wa buluu (blue economy) huku akibainisha kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za baharini ambazo bado hazijatumiwa kikamilifu.
“Kupitia usaidizi wa Afreximbank, Tanzania inaweza kuendeleza sekta hii kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.”
Kuhusu nishati safi, Waziri Mkuu alimweleza Dkt. Elombi kwamba Tanzania hivi sasa imeweka msisitizo katika matumizi ya nishati mbadala hivyo itakuwa vema endapo benki hiyo itaunga mkono juhudi hizo ili kuongeza wigo wa matumizi ya nishati hiyo kwa maendeleo endelevu.
“Pamoja na haya tunaamini Afreximbank itaendelea kupanua wigo wa kuisaidia Tanzania katika nyanja mbalimbali za maendeleo, benki hii ni mshirika wa kweli katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kati unaojali watu wake.”
Waziri Mkuu amesema kuwa hadi sasa, Tanzania imenufaika kwa kiasi kikubwa kutokana na msaada wa kifedha na kiufundi kutoka Afreximbank kwenye miradi ya Umeme wa Maji wa Julius Nyerere, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) Lot 1 na 2 na Lot 3 na 4, mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACCOP), kusaidia biashara kupitia benki za Tanzania na sekta binafsi na kusaidia bajeti za kitaifa kwa kipindi cha 2019 hadi 2024.
Benki Kuu ya Tanzania kwa sasa inamiliki hisa 2,323, ambazo ni sawa na asilimia 1.06 ya mtaji wa benki hiyo.
Kwa upande wake, Rais Mteule wa Benki ya Afreximbank, Dkt. Elombi ameiagiza timu ya watendaji wa benki hiyo ihakikishe inakamilisha kwa haraka taratibu zote zinazohusu ujenzi wa African Medical Centre of Excellence nchini Tanzania ili mradi huo mkubwa wa afya uanze kutekelezwa mapema na utoe huduma bora za matibabu ya kibingwa barani Afrika.
Pia Dkt. Elombi ametoa wito kwa Serikali ya Tanzania kuendelea kuhakikisha kuwa fedha zinazotolewa na benki hiyo zinatumika kikamilifu kwa ajili ya miradi ya maendeleo yenye tija kwa wananchi ili malengo ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii yaweze kufikiwa.
Rais huyo Mteule ameongeza kuwa ahadi na mikataba yote ya ushirikiano iliyowekwa na mtangulizi wake zitaendelea kutekelezwa kikamilifu.
Mapema, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji wa SMZ, Bw. Shariff Ali Sharriff alisema kuwa Tanzania italitumia Jukwaa la Nne la Kibiashara na Uwekezaji kati ya Afrika na Karibiani (ACTIF2025) lililoratibiwa na Afreximbank kuimarisha ushirikiano kwenye uchumi wa buluu, ushirikiano maalumu wa taasisi za uwekezaji na za kukuza biashara pamoja na sekta za anga na utalii.
“Tutahakikisha haya tutakayokubaliana hapa yanainufaisha nchi yetu,” alisisitiza.
Naye, Kamishna wa Uchambuzi wa Sera kutoka Wizara ya Fedha, Dkt. Johnson Nyela alisema kuwa Tanzania na Afreximbank zinaendelea na majadiliano kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Uuzaji Bidhaa Nje Afrika (FEDA) ili kuhakikisha wanatakeleza ujenzi wa kituo cha umahiri wa tiba barani Afrika nchini Tanzania.
“Tanzania tupo tayari kupokea mradi huu, na tunaamini tukifanikiwa kuwekeza katika eneo hilo, tutakuwa ni moja ya kitovu kikubwa cha matibabu Afrika.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi, Bw. Gilead Teri alisema mamlaka hiyo imepanga kujenga kongani ya viwanda kwa kushikirikiana na Afreximbank ambayo imelenga kuvutia uwekezaji katika sekta ya viwanda mbalimbali nchini.
Post a Comment