Ili kuendana na Dira ya Taifa 2050, Serikali ya awamu sita imedhamiria kuijenga upya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ili kuwezesha huduma zote kutolewa ndani ya jengo moja ambapo hospitali hiyo itakuwa ni mifumo ya kisasa ili kuendena na mapinduzi ya teknolojia ya tiba duniani.
Hayo yameelezwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Dkt. Delilah Kimambo wakati wa mahojiano na shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) juu uwekezaji wa miundombinu na vifaa tiba Hospitali ya Taifa Muhimbili wakati wa serikali ya awamu ya sita na kueleza kuwa mradi ambao utagharimu USD .468 Mil (takriban TZS. 1.23 Trilioni) ambapo kati ya fedha hizo USD.364 Mil zitatoka Korea Kusini.
“Tutakwenda kuweka jiwe la msingi la tatu. Itajengwa hospitali kubwa tena ya kisasa kabisa hapa Muhimbili Upanga na itaongeza huduma kwa kiwango kikubwa sana. Kwa mfano, kwa huduma ya mama mtoto pekee tutakuwa na vitanda zaidi ya 350, na vitanda vyote hivyo siyo kwamba ni kwa ajili ya huduma zile za kawaida, hapana, sisi tutakuwa tunatoa zile za kibobezi. Kwa hiyo utaona uwezekaji huo ulivyo na manufaa makubwa” amesema Dkt. Kimambo.
Kwa upande mwingine, Dkt. Kimambo ameeleza kuwa licha ya juhudi kubwa za uwekezaji ambazo zimeelekezwa katika ujenzi wa majengo mapya, ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa, pamoja na kuboresha mifumo ya usimamizi wa huduma katika hospitali, bado kuna hatua zaidi zinazochukuliwa ili kuboresha huduma kwa wananchi.
Aidha ameainisha kuwa Muhimbili mpya inatarajiwa kuongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa kulaza wagonjwa, ambapo idadi ya vitanda itaongezeka kutoka 1,500 vya sasa hadi kufikia 1,775 huku teknolojia ya kisasa kama akili unde ikitarajiwa kurahisisha utoaji wa huduma.

Post a Comment