TAASISI ZA UMMA KUKUTANISHWA KUJENGA UCHUMI SHINDANI ARUSHA



::::::::

Ofisi ya Msajili wa Hazina imeandaa kikao kazi maalum kinachojulikana kama CEO Forum 2025, kwa lengo la kuimarisha mchango wa taasisi za umma katika ujenzi wa uchumi wa kisasa unaoongozwa na matokeo.

Kikao hicho kinatarajiwa kufanyika kuanzia Agosti 23 hadi 26, 2025, jijini Arusha, kikihusisha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wapatao 700 kutoka taasisi zote za umma nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mapema leo, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Utendaji, Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bi. Lightness Mauki, alisema mkutano huo unalenga kujadili nafasi ya taasisi za umma katika mazingira mapya ya kiuchumi, kiteknolojia na kisera duniani.

Alisema kupitia mkutano huo, Serikali inatarajia kuongeza ufanisi, uwajibikaji na ubunifu wa taasisi hizo ili ziweze kushindana kimataifa, kuongeza mapato yasiyo ya kodi, na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.

“Serikali, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, inaendelea kuimarisha juhudi za mageuzi ndani ya taasisi za umma kwa kuandaa jukwaa hili la kimkakati. Lengo ni kuimarisha mawasiliano, mshikamano na kuweka dira ya pamoja kati ya bodi na menejimenti,” alisema Bi. Mauki.

Mkutano huo ni sehemu ya mwendelezo wa mageuzi yaliyoanzishwa miaka mitatu iliyopita kupitia CEO Forum, kwa kutambua kuwa taasisi za umma haziwezi tena kujiendesha kwa mifumo ya zamani isiyokidhi ushindani wa kisasa.

Kwa mujibu wa Bi. Mauki, mkutano wa mwaka huu umebeba kaulimbiu isemayo:
“Ushirikiano Endelevu wa Kibiashara Katika Mazingira Shindani Kimataifa – Nafasi ya Mashirika ya Umma.”

Alisema kaulimbiu hiyo inasisitiza umuhimu wa mashirika ya umma kubadilika kimuundo na kiutendaji ili kuchangia kwa ufanisi katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati wa juu, wenye Pato la Taifa la dola trilioni 1 na pato la mtu mmoja mmoja la dola 7,000 kwa mwaka.

“Taasisi za umma zinapaswa kuwa wabia wa kweli wa maendeleo. Tunahitaji mifumo mipya ya usimamizi, maadili bora ya kiuongozi na mazingira yanayowezesha uwajibikaji na ubunifu,” alieleza Bi. Mauki.

Aidha, alisema mkutano huo utatoa fursa ya kujifunza kutoka kwa taasisi zilizofanikiwa, huku pia ukijadili changamoto na fursa zilizopo, kwa lengo la kuleta mageuzi yenye matokeo chanya kwa Taifa.

Kwa msingi huo, Ofisi ya Msajili wa Hazina imetoa wito kwa wadau wote wakiwamo sekta binafsi, vyombo vya habari, washirika wa maendeleo na wananchi kwa ujumla, kuunga mkono juhudi hizo ili kujenga mashirika bora ya umma kwa maendeleo endelevu ya Taifa.











           PICHA ZOTE NA JAMES SALVATORY




0/Post a Comment/Comments