UAGIZAJI MAFUTA NCHINI WAPANDA, PBPA YAJIVUNIA MAFANIKIO

:::::::

Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) umetangaza kuongezeka kwa kiwango cha mafuta yanayoagizwa nchini kupitia Mfumo wa Uagizaji wa Pamoja (Bulk Procurement System - BPS), hatua inayoashiria mafanikio ya mfumo huo katika kuboresha upatikanaji wa nishati nchini na kanda ya Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa PBPA, Erasto Mulokozi, amesema kiwango cha mafuta kilichoagizwa kupitia BPS kimeongezeka kutoka wastani wa tani 5,805,193 mwaka 2021 hadi kufikia tani 6,365,986 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 9.6.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Agosti 7, 2025, katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mulokozi alisema matarajio ni kwamba hadi kufikia mwisho wa mwaka huu, kiasi hicho kitaongezeka hadi tani 7,090,165, ongezeko la asilimia 11.4 kutoka mwaka uliopita.

"Kuongezeka kwa ufanisi katika utekelezaji wa mfumo huu kumesaidia kujenga imani kubwa kwa nchi jirani zinazotegemea Tanzania kama kitovu cha uagizaji mafuta," alisema Mulokozi.

Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2021, Tanzania iliagiza tani milioni 5 za mafuta, ambapo tani milioni 2 ziliuzwa kwa mataifa jirani na tani milioni 3 kutumika ndani ya nchi. Mwaka uliofuata (2022), zaidi ya tani milioni 6 ziliagizwa, huku tani milioni 3 zikienda kwa nchi jirani na takribani tani milioni 2.5 kwa matumizi ya ndani.

Mwaka 2024, kiwango hicho kilipanda tena, zaidi ya tani milioni 6 zikiagizwa—tani milioni 3 kwa matumizi ya ndani na kiasi kinachozidi milioni 3 kwa mataifa jirani. Tangu Januari hadi Septemba 2025, tani zaidi ya milioni 5 zimeshawasili nchini, ambapo tani milioni 3 zilisafirishwa kwenda nchi jirani huku zaidi ya milioni 2 zikitumika ndani ya Tanzania.

Kwa mujibu wa PBPA, idadi ya kampuni za mafuta zinazoshiriki kwenye mfumo huo imeongezeka kutoka 33 mwaka 2021 hadi 73 mwaka huu. Ongezeko hilo linachangia fursa mpya za ajira kwa Watanzania katika sekta ya nishati na usafirishaji.

Aidha, mataifa jirani kama Zambia, Burundi, Rwanda, Malawi, na Kenya yameonyesha kuvutiwa na mfumo huo na kuja kujifunza kutokana na mafanikio yake, jambo linalodhihirisha Tanzania kuwa kinara wa ubunifu na usimamizi bora katika sekta hiyo.

“Mafanikio haya si ya PBPA pekee, bali ya taifa zima. Ni fahari kuona mataifa mengine yanajifunza kutoka kwetu," alisema Mulokozi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bw. Sabato Kosuri, alisema kuwa serikali inaendelea kuthamini mchango wa vyombo vya habari katika uelimishaji wa umma na kuimarisha uzalendo kupitia taarifa sahihi.

Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),  Deogratius Balile, alipongeza hatua zilizofikiwa kupitia mfumo huo na kusisitiza umuhimu wa kuhakikisha ubora wa mafuta unaoingizwa nchini unadhibitiwa ipasavyo.












 

0/Post a Comment/Comments