Benki ya CRDB imefanya maboresho makubwa ya mfumo wake wa kidigitali ili kuimarisha utoaji wa huduma na kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia ya kimataifa.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela, amesema maboresho hayo yamehusisha kubadilisha mfumo wa zamani na kuweka mfumo mpya wenye uwezo wa kutoa huduma kwa ufasaha, kuongeza usalama wa miamala na kurahisisha upatikanaji wa huduma kote nchini na nje ya Tanzania.
Nsekela ameeleza kuwa mabadiliko hayo yalihusisha pia nchi jirani kama Burundi, na ni sehemu ya mafanikio makubwa yanayoadhimisha miaka 30 ya benki hiyo na kuwa wakati wa utekelezaji wa maboresho hayo, baadhi ya matawi yalipata changamoto za utoaji huduma, lakini taarifa ziliwafikia wateja kwa wakati na hivyo kuepusha taharuki na huduma za ushauri na SimBanking ziliendelea kama kawaida na sasa mifumo yote imerejea kikamilifu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mifumo kutoka CRDB, Bruce Mwire, amesema maboresho hayo yalilenga kuhakikisha kuwa mfumo mpya unakidhi viwango vya kimataifa na unazingatia zaidi usalama wa wateja na kubainisha kuwa mfumo huo unashikilia zaidi ya asilimia 25 ya miamala nchini, hivyo suala la kuimarisha ulinzi wa taarifa na miamala ya wateja limepewa kipaumbele cha kwanza.
Mfumo mpya utawezesha benki kuhimili mabadiliko ya teknolojia yanayokuja, kutoa huduma kwa lugha anayoitumia mteja, na kuimarisha diplomasia ya kiuchumi kupitia huduma bora za kifedha,na kuwa uwekezaji huo ni endelevu na umehusisha ushirikiano na wataalamu kutoka mataifa mbalimbali, jambo linaloiweka CRDB kwenye nafasi ya kuendelea kuongoza sekta ya fedha barani Afrika.
Post a Comment