LHRC NA NORWAY WASAINI MKATABA MPYA WA MAKUBALIANO

:::::::::::::

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway nchini,  wamesaini mkataba mpya wa makubaliano ya ushirikiano wa miaka mitatu wenye thamani ya Krone milioni 19 za Norway, sawa na takribani dola milioni 2 za Kimarekani.

Makubaliano hayo yamefikiwa katika hafla rasmi iliyofanyika katika ofisi za makao makuu ya LHRC zilizopo Kijitonyama, jijini Dar es Salaam, ambapo viongozi kutoka pande zote mbili, wawakilishi wa mashirika ya kiraia na wanahabari walihudhuria.

Akizungumza katika tukio hilo, Balozi wa Norway nchini Tanzania, Tone Tinnes, alieleza kuwa mkataba huo unaendeleza uhusiano wa muda mrefu kati ya Norway na LHRC katika kusimamia haki za binadamu hapa nchini.

“Kupitia makubaliano haya, Norway inaendeleza dhamira yake ya kuunga mkono misingi ya haki, maridhiano ya kisiasa, usawa wa kijinsia, pamoja na uhuru wa kujieleza – ambayo yote ni msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi,” alisema Balozi Tinnes.

Aliongeza kuwa haki za kisiasa na maridhiano ya kijamii ni nguzo muhimu za kujenga imani miongoni mwa wananchi, na kwamba taifa lolote lenye misingi imara ya demokrasia linahitaji uhuru wa maoni na sauti huru za kiraia.

Kwa upande wa LHRC, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Wakili Fulgence Massawe, alisema makubaliano hayo yanatoa msukumo mpya katika utekelezaji wa mkakati wa taasisi hiyo wa miaka mitano (2025–2030), hasa katika kipindi cha awali cha utekelezaji wake.

“Huu ni muendelezo wa uhusiano madhubuti kati ya LHRC na Norway, uhusiano ambao tangu mwaka 2013 umesaidia katika maeneo mbalimbali kama mageuzi ya sheria, msaada wa kisheria kwa wananchi na mashauri ya kimkakati,” alieleza Wakili Massawe.

Tangu kuanza kwa ushirikiano huo zaidi ya muongo mmoja uliopita, Norway imetoa zaidi ya NOK milioni 61 kufanikisha shughuli mbalimbali za LHRC, ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushiriki wa wananchi katika masuala ya uwajibikaji kitaifa na kimataifa.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka LHRC, mkataba huu mpya unalenga kutoa msukumo katika maeneo ya haki jinai, sheria za uchaguzi, pamoja na kuhakikisha ushirikishwaji wa wanawake na makundi mengine yaliyo pembezoni katika mchakato wa haki na maendeleo.
















 

0/Post a Comment/Comments