MGOMBEA UBUNGE CCM CHATO KASKAZINI KUANZA NA SOKO KUU

Mgombea Ubunge kupitia CCM Jimbo la Chato Kaskazini akiomba kura kwa wananchi.Mgombea Ubunge Jimbo la Chato Kaskazini, Mwl. Cornel Magembe,akiomba kura kwa wananchi wa Jimbo hilo.

........

MGOMBEA Ubunge Jimbo la Chato Kaskazini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mwl.Cornel Magembe, ameahidi kuanza na ujenzi wa soko kuu la wilaya ya Chato mkoani Geita iwapo atachakuguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo hilo katika Uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

Soko hilo linatazamiwa kujengwa kwenye Kata ya Muungano ilipokuwa stendi ya mabasi kwa lengo la kuinua uchumi wa wananchi ikiwemo wajasiliamali.

Mbali na hilo, pia amesema hatokuwa Mbunge wa kusinzia Bungeni na kwamba atahakikisha anaeleza kero za wananchi wa Jimbo hilo na kwamba hataogopa kuzungumza mambo magumu ambayo ni kwa maslahi ya wananchi.

 Kadhalika amewataka wananchi kumpigia kura nyingi mgombea Urais wa chama hicho, Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aweze kuendeleza maendeleo mengi yaliyoanzishwa na mtangulizi wake Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, na yale mapya aliyoyaanzisha katika utawala wa serikali ya awamu ya tano.

Alikuwa kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za Uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani 2025 katika Jimbo la Chato Kaskazini uliofanyika kwenye stendi ya zamani mjini Chato.

Aidha Mwl. Magembe amewahakikishia wananchi kuwa baadhi ya ndoto za Hayati Dkt. Magufuli ikiwemo ujenzi wa Chuo cha Udaktari kwenye Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato kitajengwa na kukamilika pasipo mashaka yoyote.

Mbali na Mwl. Magembe, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Chato Kusini, Paschal Lutandula, amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kuwachagua wagombea wanaotokana na CCM kwa madai ndiyo Chama pekee chenye nia ya dhati ya kuwaletea maendeleo wananchi.

Vilevile amesema uwepo wa wabunge wawili kwenye wilaya ya Chato itasaidia kuharakisha maendeleo ya wananchi ikiwa ni pamoja na kuitangaza vyema hifadhi ya Burigi Chato ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kiwanja cha ndege cha mkoa wa Geita kilichopo wilayani chato kinaeendea kutoa huduma kama ilivyokuwa ndoto ya Rais Hayati Dkt. Magufuli.

Katika ufunguzi wa kampeni hizo baadhi ya viongozi mbalimbali wamehudhuria akiwemo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Geita,viongozi wa wilaya ya Chato, wasanii mbalimbali akiwemo Chege Chigunda, Madee na Magambo Machimu, ambao wametoa burudani mbalimbali.

                          Mwisho.


 

0/Post a Comment/Comments