Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kutoa mafunzo kuhusu ubora, viwango na kanuni za uongezaji virutubishi kwenye mazao ya chakula ikiwemo mahindi, ngano, chumvi na mafuta yaliyosafishwa, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Kanuni ya mwaka 2024,Mafunzo hayo yamefanyika leo jijini Dar es Salaam yakilenga kuwajengea uwezo wazalishaji, wasambazaji na wauzaji ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinakidhi viwango vya kitaifa.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TBS, David Ntibarema amesema kanuni mpya zimeandaliwa ili kuwezesha uzalishaji wa bidhaa bora zenye virutubisho vinavyokidhi mahitaji ya lishe na usalama wa walaji na kuwa mafunzo hayo yameanza katika mkoa wa Dar es Salaam katika wilaya za Ubungo, Kinondoni na Temeke na yataendelea hadi Septemba 16 kabla ya kufanyika katika mikoa mingine nchini.
Ntibarema amesisitiza umuhimu wa wazalishaji na wasambazaji kuzingatia kanuni hizo kwa makini ili kuhakikisha bidhaa zinazotoka viwandani zinakuwa na ubora unaotakiwa,na kuongeza kuwa baadhi ya changamoto zilizobainishwa na wazalishaji, ikiwemo suala la matumizi ya nembo, zinahitaji kushughulikiwa kwa kufuata mwongozo rasmi wa TBS.
Kwa mujibu wa washiriki wamesema kuwa mafunzo haya yatawasaidia wadau wa sekta ya chakula kuongeza uelewa wa viwango na kujenga uwezo wa kuzalisha bidhaa zenye ushindani zaidi sokoni na wameshauriwa kushiriki kikamilifu ili kuhakikisha elimu wanayoipata inatafsiriwa moja kwa moja kwenye shughuli zao za kila siku za uzalishaji na usambazaji.
Post a Comment