WIZARA YA AFYA YATOA VITENDEA KAZI KWA WATOA HUDUMA ZA AFYA NGAZI YA JAMII

Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Bi. Zuwena Omary (wa tatu kutoka kushoto) akiwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe (wa pili kushoto) akikabidhi vyeti na vitendea kazi kwa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHW) waliohitimu mafunzo katika hafla iliyofanyika leo Septemba 8, 2025, katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Lindi, Mkoani Lindi (PICHA NA NOEL RUKANUGA)

Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Bi. Zuwena Omary akizungmza katika hafla ya kukabidhi vyeti na vitendea kazi kwa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHW) waliohitimu mafunzo katika hafla iliyofanyika leo Septemba 8, 2025, katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Lindi, Mkoani Lindi.

Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe akizungmza jambo katika hafla ya kukabidhi vyeti na vitendea kazi kwa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHW) waliohitimu mafunzo katika hafla iliyofanyika leo Septemba 8, 2025, katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Lindi, Mkoani Lindi.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Dkt. Kheri Kagya akizungmza katika hafla ya kukabidhi vyeti na vitendea kazi kwa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHW) waliohitimu mafunzo katika hafla iliyofanyika leo Septemba 8, 2025, katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Lindi, Mkoani Lindi.

Kaimu Mkurugenzi wa Mradi wa Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation, Bi. Zawadi Dakika akitoa salamu za wadau wa maendeleo katika hafla ya kukabidhi vyeti na vitendea kazi kwa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHW) waliohitimu mafunzo katika hafla iliyofanyika leo Septemba 8, 2025, katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Lindi, Mkoani Lindi.

Mhitimu wa mafunzo ya huduma ya Afya ngazi ya Jamii Bw. Dickson Maluchila akitoa shukrani kwa Serikali na wadau wa sekta ya afya kwa niaba ya wahitimu wezake katika hafla ya kukabidhi vyeti na vitendea kazi kwa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii iliyofanyika Mkoani Lindi.

Baadhi ya wadau mbalimbali sekta ya afya wakiwa katika hafla ya hafla ya kukabidhi vyeti na vitendea kazi kwa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii

Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Bi. Zuwena Omary (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wa mafunzo ya huduma ya Afya ngazi ya Jamii.

...........................

NA NOEL RUKANUGA, LINDI

Wizara ya Afya imekabidhi vitendea kazi kwa wahudumu wa afya 3,561 waliohitimu mafunzo ya kutoa huduma ya Afya ngazi ya Jamii (CHW) mkoani Lindi ili kuboresha miundombinu, kuimarisha utoaji wa huduma katika sekta ya afya ngazi ya jamii, jambo ambalo litasaidia kutatua changamoto katika sekta hiyo, ikiwemo wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya afya.

Hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa utekelezaji katika kipindi cha miaka mitano ambapo Wizara ya Afya imekusudia kusomesha watu 137,000 kwa ajili ya kutoa huduma ya afya ngazi ya jamii ili kuongeza nguvu katika kutoa elimu na huduma ya afya, kinga, lishe, huduma za mama na mtoto, tiba za awali.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vyeti na vitendea kazi kwa wahudumu wa afya ngazi ya Jamii (CHW) waliohitimu mafunzo, iliyofanyika Septemba 8, 2025, katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Lindi, Mgeni rasmi wa hafla hiyo, ambaye ni Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Bi. Zuwena Omary, amesema kuwa mpango wa Serikali ni kuhakikisha kila mtu anafikiwa na huduma bora ya afya kwa kupitia wahudumu wa ngazi ya jamii.

Bi. Zuwena amesema kuwa mpango wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii ulizinduliwa mwaka 2024 na Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango, japo miaka 1970 ulikuwa unatumika lakini ulisimama kutokana na changamoto, hivyo kwa sasa programu hiyo imeboreshwa ili kuleta tija iliyokusudiwa.

"Naomba tuzingatie miongozo ya namna ya kuwapata watoa huduma ya afya ngazi ya jamii, ambao watakuwa na uwezo na utashi wa kufanya kazi katika vijiji na vitongoji, katika mikoa ambayo hawajachagua watu kwa ajili ya kwenda katika mafunzo ya" amesema Bi. Omary.

Amefafanua kuwa wahitimu wa mafunzo hayo wanakwenda kuleta manufaa makubwa, ikiwemo kupunguza vifo na kuepuka kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya afya.

"Serikali itawapatia posho, vifaa vya kazi. Naiomba jamii ya Watanzania kutoa ushirikiano na kuthamini mchango wa watoa huduma za afya ngazi ya jamii," amesema Bi. Omary.

Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, amesema kuwa watoa huduma ngazi ya jamii katika sekta ya afya ni kama jeshi ambalo linachangia kwa kiasi kikubwa kuhakikisha malengo ya sekta ya afya yanafikiwa.

Dkt. Magembe amesema kuwa watoa huduma wa Afya ngazi ya Jamii wamepatiwa mafunzo kwa muda wa miezi sita, hivyo wanatarajiwa kuwa daraja kati ya vituo vya tiba na wananchi katika kuhakikisha huduma inatolewa kwa ufanisi.

"Mnatakiwa kutekeleza majukumu yenu mliopangiwa kwa kufuata miongozo, Tunawategemea ninyi katika kuhakikisha mnakwenda kutoa huduma bora ya afya," amesema Dkt. Magembe.

Amesisitiza umuhimu wa wahitimu kuzingatia maadili ya kazi, kutumia lugha rafiki ya kuongea na wateja, kuepuka kutoa huduma kwa upendeleo, kulinda siri za wagonjwa, huku akibainisha kuwa Serikali itaendelea kutengeneza mazingira rafiki katika sekta ya afya.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Dkt. Kheri Kagya, amesema kuwa wahitimu hao wanakwenda kuwa msaada mkubwa wa kuimarisha utoaji wa huduma za afya katika mkoa huo, hususani katika maeneo ya lishe, mazingira, afya ya uzazi, pamoja na kuwa kiungo muhimu kwa jamii.

Dkt. Kagya amesema kuwa wahitimu hao wamepatiwa vitendea kazi mbalimbali, ikiwemo vishikwambi pamoja na baiskeli 643 za kisasa, kwa ajili ya kuwasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Akitoa salamu za wadau wa maendeleo, Kaimu Mkurugenzi wa Mradi wa Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation, Bi. Zawadi Dakika, amesema kuwa katika kutekeleza mpango huo wa Kitaifa wa Jumuiya wa huduma ya afya ngazi ya jamii, taasisi hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya kupitia ufadhili wa Global Fund, imefanikiwa kuwezesha Kamati za Kitaifa inayosimamia huduma za afya ngazi ya jamii.

Dakika amesema kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo wataendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha jamii inaendelea kupata huduma bora ya afya katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza kwa niaba ya wahitimu Bw. Dickson Maluchila, wameahidi kufanya kazi kwa moyo, nidhamu, na bidii kwa kuzingatia miongozo ya Serikali pamoja na uadilifu kwa kulenga kutoa elimu na huduma ya afya, kinga, lishe, huduma za mama na mtoto, vijana pamoja na makundi maalum.

"Tutakuwa mstari wa mbele katika kupunguza magonjwa na kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa ukaribu na wakati, pamoja na kuwa mabalozi bora wa afya, usafi wa mazingira, utunzaji wa afya ya jamii na familia kwa ujumla," amesema.

Ameishukuru Serikali pamoja na wadau sekta ya afya kwa kuwapatia mafunzo na vitendea kazi, huku akieleza kuwa wanatambua jukumu waliokuwa nalo si dogo, lakini wapo tayari kulitumikia Taifa kwa moyo wa dhati na kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya afya ngazi ya jamii.

Katika hafla hiyo ya utoaji vyeti wahitimu 222 kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Lindi walishiriki kwa niaba ya wengine waliohitimu mafunzo hayo kutoka mikoa 12 nchini.

Serikali imefanikiwa kuwawezesha wahitimu wa mafunzo ya huduma ya Afya ngazi ya Jamii, vitendea kazi mbalimbali ikiwemo vishikwambi, mizani, vipima joto, mabegi, nyavuli, mabuti, pamoja na vifaa vya kupimia huduma ya afya ya lishe.

0/Post a Comment/Comments