Naibu Waziri wa Fedha
na Mipango, Mhe. Hamad Yussuf Masauni (Mb) (kulia) akieleza kuhusu Benki Kuu ya
Tanzania (BoT) kuwa na mbinu za kibunifu katika kuhifadhi dhahabu na
kukuza sekta zinazoongeza fedha za kigeni, wakati alipotembelea BoT, ikiwa ni
muendelezo wa ziara ya kutembelea taasisi zilizo chini ua Wizara hiyo, kushoto
ni Naibu Gavana wa BoT, Dkt. Bernard Kibesse. 
Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Bernard Kibesse, akifafanua jambo wakati wa mkutano kati ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Yussuf Masauni (Mb) (hayupo pichani) na Viongozi wa BoT wakiwemo Manaibu Gavana na Wakurugenzi, jijini Dar es Salaam.
Naibu Gavana wa Benki
Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Julian Banzi Raphael, akieleza majukumu ya Benki
hiyo hususani katika eneo la utawala na udhibiti wa ndani, wakati wa mkutano
kati ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Yussuf Masauni (Mb)
(katikati) na Viongozi wa BoT wakiwemo Manaibu Gavana na Wakurugenzi, jijini
Dar es Salaam, kushoto ni Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt.
Bernard Kibesse.
Mkurugenzi wa Utafiti
na Sera za Uchumi, wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Suleiman Missango
(kushoto), akieleza majukumu yake yakiwemo ya kutoa ushauri, kuandaa Sera na
kuangalia mwenendo wa utekelezaji wa Bajeti, wakati wa mkutano kati ya Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Yussuf Masauni (Mb) (hayupo pichani) na
viongozi wa BoT wakiwemo Manaibu Gavana na Wakurugenzi, jijini Dar es Salaam.
Na. Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Fedha
na Mipango, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania
(BoT) itekeleze haraka maelekezo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan hivi karibuni kuhusu Taasisi za Fedha kupunguza
riba za mikopo ili kuwawezesha wafanyabiashara na watanzania kwa ujumla kukopa
na kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.
Mhe. Masauni ametoa
maagizo hayo alipotembelea Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Jijini Dar es Salaam na
kufanya mazungumzo na Uongozi wa Benki hiyo ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake
za kutembelea Taasisi zilizochini ya Wizara ya Fedha na Mipango.
Alipongeza jitihada
zinazofanywa na Benki Kuu ya Tanzania za kukutana na wadau ili kuhakikisha kuwa
Taasisi za Fedha zikiwemo Benki na Watoa huduma wa Sekta Ndogo ya Fedha
wanapunguza riba za mikopo yao ili kuwawezesha wananchi kupata mikopo isiyo na
gharama kubwa.
“Niwapongeze kwa
juhudi zilizoanza kuchukuliwa kuwezesha riba kupungua na ikiwezekana mwishoni
mwa mwezi huu wananchi waanze kuona matokeo ya juhudi hizo kwa riba kuanza
kupungua, kwa kuwa kupungua kwa riba ni jambo linalowezekana”, alieleza
Mhandisi Masauni.
Aidha, ameitaka Benki
hiyo kuhakikisha inaweka mikakati mahususi ya kuongeza akiba ya Fedha za kigeni
kwa kuwa na mbinu za kibunifu zikiwemo kuanza kununua na kuhifadhi dhahabu
pamoja na kuongeza uuzaji wa bidhaa za Tanzania nje ya nchi na kusimamia kikamilifu
shughuli za utalii.
Kuhusu suala la fedha
za wananchi waliokuwa wateja wa Benki ya FBME Limited iliyowekwa chini ya
uangalizi wa Bima ya Amana za Wateja inayosimamiwa na Benki Kuu ya
Tanzania ikiwa katika hatua za kufilisiwa, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Hamad Yussuf Masauni, ameitaka Benki hiyo kuhakikisha wateja wa Benki hiyo
wanarejeshewa fedha zao haraka baada ya kukamilisha taratibu za kisheria
zinazoendelea nchini Cyprus.
Kwa upande wake Naibu
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Bernard Kibesse, alimhakikishia
Mhe. Naibu Waziri Masauni kwamba Benki yake inakamilisha mazungumzo na mabenki
ili washushe riba kama alivyoelekeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan jijini
Mwanza.
Alisema Benki Kuu pia
inaendelea kurekebisha kanuni mbalimbali za mikopo inayotolewa na Benki hiyo
kwa Mabenki ili kuziongezea ukwasi Benki hizo ili na zenyewe zitumie fursa hiyo
kushusha riba za mikopo.
Aidha, Naibu Gavana
Dkt. Kibese alieleza kuwa Benki Kuu ya Tanzania itaanza kununua na kuhifadhi
dhahabu baada ya Kiwanda cha kuchakata dhahabu cha Mwanza kilichozinduliwa na
Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan jijini Mwanza hivi karibuni kupata hati ya
uthibitisho ya uzalishaji wa dhahabu wa viwango vya kimataifa ambavyo ili cheti
hicho kitolewe, kiwanda kinatakiwa kuzalisha dhahabu yenye ubora wa asilimia
99.9.
Naibu Waziri wa Fedha
na Mipango Mhandisi Masauni yupo jijini Dar es Salaam katika ziara yake kikazi
ambapo atatembelea ofisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango.
Mwisho


Post a Comment