Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi amelitaka Baraza la Michezo nchini (BMT) kujiandaa kuanza kuratibu kimkakati zaidi masuala ya michezo ikiwemo fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Michezo.
Dkt. Abbasi ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa kikao na BMT kujadili miongozo mbalimbali ambayo inaandaliwa na Baraza hilo likielekea katika uratibu wa kimkakati zaidi wa michezo nchini. Baadhi ya miongozo iliyojadiliwa ni ule wa uingizaji wa nyasi bandia ambao umepewa msamaha wa kodi na mwongozo kuhusu Serikali kusaidia michezo hasa Timu za Taifa kama alivyoagiza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
“Miongozo hii tunatakiwa kuikamilisha mwezi huu wa Julai, 2021 ili wadau wajue nini cha kufanya wakati huu ambapo Serikali ya Awamu ya Sita inafanya mageuzi makubwa na ya kihistoria katika uendeshaji, usimamizi na ufadhili wa michezo nchini,” alisema Dkt. Abbasi.

Post a Comment