Haki ni stahiki za kisheria ambazo mtu anapaswa azipate au apewe.
Wajibu ni majukumu ambayo mtu anapaswa kuyatimiza katika kufanikisha au kukamilisha jambo fulani. Katika makubaliano ya mkopo haki za mkopaji ni wajibu kwa mkopeshaji na wajibu wa mkopaji huwa ni haki kwa mkopeshaji. Kwa hiyo kila upande utapaswa kuhakikisha kuwa unatimiza wajibu wake ili kukamilisha makubaliano hayo na kuyafanya yawe halali kisheria pasipo kuwepo kwa kikwazo cha aina yoyote.
Katika makubaliano ya mkopo, mkopaji unapaswa kutambua sio tu haki zako bali pia na wajibu wako kisheria. Kutimizwa kwa wajibu wako ndiko kutakako kupa nguvu za kudai haki zako.
Moja kati ya haki zako za msingi ni kufahamu unaingia katika makubaliano ya mkopo ya aina gani. Hii ina maana kuwa, usikubali kukopeshwa kienyeji bila kufahamu hasa makubaliano hayo yakoje. Sheria ya Mikataba Sura ya 345 kama ilivyorejewa mwaka 2002 inamtaka kila anayeingia kwenye makubaliano ya mkopo kutambua uhalisia wa aina ya makubaliano anayoingia. Usikubali tu kusaini nyaraka ambazo huelewi zimeandikwa nini. Usikubali tu kupokea fedha ambazo hujui madhara yake ni nini. Fedha inayopatikana kirahisi sana, hupotea kirahisi sana tena kwa majuto makubwa.
Hakikisha unapata muda wa kutosha kuusoma mkataba wako wa mkopo ili ufahamu haki zako ni zipi na wajibu wako ni upi kisheria. Ukiona huelewi kilichoandikwa ni vyema ukamtafuta mtu mwenye uelewa au wakili ili akusaidie kukuelewesha. Usijifanye unajua wakati hujui lolote.
Mkopaji pia una haki ya kuuliza maswali ya kila aina yatakayokupa mwangaza wa aina gani ya makubaliano unayoingia. Kuuliza si ujinga, tumia haki hiyo upate ufahamu wa kutosha kabla hujakopa. Fahamu pia sheria imeagiza kulindwa kwa utu wako, usiri wako na heshima yako. Hata kama unadaiwa na umeshindwa kulipa, sheria haimpi haki mkopeshaji kukutukana, kukudhalilisha, kukufanyia fujo na kuingia nyumbani kwako au dukani kwako na kuvunja, kuchukua au kuuza mali zako kinguvu. Hilo ni kosa la jinai kisheria. Hata kama mkopeshaji anaweza kuwa na haki ya kuuza dhamana yako, lakini bado anapaswa kutoa taarifa ndani ya muda wa kutosha kwako na kwa uongozi wa serikali ya mtaa na kata. Wakati mwingine anapaswa apate amri au kibali cha mahakama kinamchomruhusu kufanya hivyo. Kukosekana kwa vyote hivyo huondoa uhalali wa mauzo ya mali yako kisheria.
Mkopaji pia una haki ya kupinga mauzo ya mali yako mahakamani au katika Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya endapo utagundua kuwa mauzo ya mali yako hayakufanyika kihalali. Mke au mume wa mkopaji unaweza pia kupinga mauzo ya mali ya ndoa ambayo iliwekwa dhamana bila kukushirikisha na kutoa idhini yako. Usikubali haki yako ipotee kirahisi.
Pamoja na haki zako nyingi kisheria, fahamu kuwa unao wajibu wa kutimiza. Usipotimiza wajibu wako unajinyima nguvu ya kudai haki zako. Kumbuka unawajibika kisheria kulipa mkopo kwa wakati, kutoa taarifa sahihi kwa mkopeshaji, kutunza kumbukumbu za nyaraka za mkopo wako, kumshirikisha mkeo au mumeo juu ya dhamana unayoweka rehani, kujenga mahusiano na mawasiliano mazuri na mkopeshaji na kutoa taarifa mapema za kushindwa kupeleka marejesho kwa wakati au kushindikana kabisa kulipwa kwa mkopo. Fahamu haki zako kisha utimize wajibu wako.

Post a Comment