Picha na Mtandaoni
Na Wakili Justine Kalebo
Mali za familia ni mali zilizopatikana katika muktadha wa familia kwa maana ya chini ya Muunganiko wa mume na mke ambao umepelekea kuzaliwa kwa watoto au ongezeko la watu wengine katika familia hiyo. Mali hizi hupatikana kwa jitihada za pamoja za mke na mume kila mmoja akiwa na mchango wake kwa namna moja au nyingine na baadaye watoto kushirikishwa katika mchakato huo.
Kisheria ndugu, jamaa na marafiki ni wageni ambao wanaweza kukaribishwa kusaidia katika kuchangia mawazo au nguvukazi katika kuwezesha na kufanikisha mchakato mzima wa upatikanaji wa mali hizo. Baba, Mama, Mjomba, Shangazi, Kaka, Dada au ndugu yeyote wa mke au mume hawezi kuchukua nafasi ya mume, mke au watoto katika uendeshaji na umiliki wa mali za familia.
Familia ni taasisi kamili inayojitegemea na yenye serikali yake. Kuruhusu serikali ya familia iongozwe na mtu ambaye sio mhusika mkuu wa serikali hiyo ni kuhatarisha usalama na uimara wa serikali yenyewe. Kuruhusu wazazi au ndugu waamue namna mtakavyofanya biashara na kumiliki mali zenu kama familia ni kutweza mamlaka, haki na wajibu wa kila mwana familia.
Kanuni za uendeshaji bora wa biashara pamoja na miradi mbalimbali zinaeleza kwamba, maamuzi yoyote yanayohusiana na umiliki wa mali yoyote ile au biashara inayofanywa katika ngazi ya familia, yanapaswa yaanzie kwa kujadiliwa na kutamatishwa kwenye ngazi ya familia sio kwa ndugu. Pamoja na mchango mkubwa wa ndugu katika kushauri, kuwezesha na kusaidia kufanikisha mambo mbalimbali, lakini muamuzi wa mwisho wa mustakabali wa uchumi na mali za familia anapaswa kuwa ni wana familia wenyewe.
Ni makosa makubwa kufanya biashara, kuanzisha mradi au kununua mali yoyote ile kwa shinikizo kutoka kwa wazazi au ndugu na kwa kumficha mume au mke wako pamoja na watoto na kuwashirikisha wazazi na ndugu zako tu. Hiyo ni dalili tosha kuwa serikali yako katika ngazi ya familia haiko imara. Kuruhusu ndugu, jamaa na marafiki zako wachukue nafasi kubwa katika uendeshaji wa biashara na miradi yako mbalimbali huku ukimuweka nyuma sana mke/mume pamoja na watoto wako, kunaweza kuja kukugharimu kesho na hasa utakapokuwa haupo tena duniani.
Japokuwa sio wote, lakini asilimia kubwa ya ndugu hao wanaweza kuwa miongoni mwa wale watumainio cha ndugu na mwishoni huja kufa maskini. Hawajishughulishi, hawana malengo wala mipango yoyote. Mpango wao mkubwa ni kuja kurithi mali zako tu kwa kumnyanyasa mke/mume wako pamoja na watoto wako. Wengine ni wepesi sana kuendesha familia yako na kuingilia maamuzi yenu kifamilia, lakini wao hawawezi kukushirikisha mambo yao, wala hawataki kuingiliwa katika maamuzi ya familia zao.
Mafanikio katika biashara na uchumi imara hayapatikani kwa miujiza, bali hupatikana kwa kuanza kwanza kujenga taasisi imara ya familia ambayo haiendeshwi kama gari bovu na kuyumbishwa kama bendera. Mafanikio katika biashara yanaanza kwa kuanza kuwathamini kwanza wadau wa familia yako ambao huanza na wewe tangu mwanzo wa uanzishwaji wa biashara na miradi mbalimbali. Huwezi kuwa mpole na mkarimu sana kwa wengine na na ukawa mkali, katili na mchoyo sana kwa familia yako ukategemea kufanikiwa, haiwezekani. Mke/mume na watoto wanapaswa kuwa wa kwanza kuthaminiwa na kushirikishwa katika biashara na miradi mbali mbali ili ifanikiwe.
Kwa Ushauri zaidi unaweza kufika katika ofisi zetu zilizopo, Dar es salaam, Posta Mpya, Jengo la Mavuno House, Ghorofa ya 1, Ofisi Na. 102B. Kwa mawasiliano zaidi au msaada wa kisheria, wasiliana nasi kwa anwani ifuatayo:-
Mkurugenzi Mkuu,
Moriah International Foundation,
Idara ya Msaada wa Kisheria,
P.O. Box 70849,
Dar es salaam.
Simu: +255 713 63 62 64 / +255 755 54 56 00 / +255 222 110 684
Email: jukwaalasheria@gmail.com / moriahlawyer@gmail.com
Facebook: Jukwaa la Sheria
Post a Comment