Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew
akiteta jambo na Mkuu wa Uendeshaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Mhandisi
Albert Richard wakati wa mkutano na wananchi katika Kijiji cha Vuje kilichopo
wilayani Same ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kukagua ubora na upatikanaji
wa huduma ya mawasiliano katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Kilimanjaro
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu na Mbunge
wa Same Mashariki Mhe. Anne Kilango Malecela akiteta jambo na Naibu Waziri wa
Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew wakati wa ziara ya
Naibu Waziri huyo ya kukagua ubora na
upatikanaji wa huduma ya mawasiliano katika baadhi ya maeneo ya wilaya ya Same
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew
akisikiliza kero na malalamiko ya wananchi zinazohusu mawasiliano katika Kijiji
cha Vuje kilichopo wilayani Same ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kukagua
ubora na upatikanaji wa huduma ya mawasiliano katika baadhi ya maeneo ya Mkoa
wa Kilimanjaro. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya
Miundombinu na Mbunge wa Same Mashariki Mhe. Anne Kilango Malecela na Kushoto kwake ni Mkuu wa Uendeshaji wa
Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Mhandisi Albert Richard
Mkuu wa TCRA Kanda ya Kaskazini Mhandisi Imelda Salum akizungumza na
wananchi wa Kijiji cha Vuje kilichopo Kata ya Vuje Wilayani Same wakati wa
ziara ya Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo
Mathew (hayupo pichani) ya kukagua ubora na upatikanaji wa huduma ya
mawasiliano katika wilaya hiyo
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Vuje kilichopo Kata ya Vuje Wilayani Same wakati wa ziara yake ya kukagua ubora na upatikanaji wa huduma ya mawasiliano katika wilaya hiyo
Na Mwandishi wetu, SAME
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amefanya ziara ya kukagua upatikanaji wa huduma ya mawasiliano ya simu, data na redio katika kata mbili za Vuje na Bombo zilizopo katika wilaya ya Same, jimbo la Same Mashariki na kuahidi kutatua changamoto za mawasiliano kwa wananchi kwasababu ni haki yao ya msingi na sio hisani
Katika ziara yake Mhandisi Kundo aliambatana na watendaji kutoka taasisi nne za mawasiliano zilizo chini ya Wizara hiyo ambazo ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na Shirika la Posta Tanzania (TPC) pamoja na wawakilishi kutoka katika makampuni ya simu ya Airtel, Tigo, TTCL, Halotel na Vodacom
Mhandisi Kundo alisikiliza kero na malalamiko ya wananchi kuhusu kukosekana kwa huduma ya mawasiliano ya simu za mkononi na intaneti ambazo zinasababisha athari mbalimbali za kijamii, kiuchumi pamoja na watumishi wa Serikali kupata changamoto mbalimbali za kupokea na kutuma taarifa kupitia mifumo mbalimbali ya TEHAMA
Amesema kuwa Wizara hiyo inaelewa changamoto ya mawasiliano iliyopo katika eneo hilo na tayari hatua mbalimbali zimeshaanza kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na UCSAF kutangaza awamu ya sita ya zabuni za kupeleka mawasiliano katika maeneo ya mipakani ambapo katika jimbo la Same Mashariki minara itajengwa katika vijiji vya Mbwambo, Ugwama na Mwatemi
Naye Mkuu wa Uendeshaji wa UCSAF Mhandisi Albert Richard amesema kuwa baada ya kufika katika eneo la kata ya Vuje Kijiji cha Vuje amekuta kuna mnara wa simu wa Airtel lakini bado hali ya mawasiliano sio nzuri na kuahidi kuyaomba makampuni ya simu kuweka vifaa vyao kwenye mnara wa Airtel uliopo ili huduma ya mawasiliano ya mitandao mingine iweze kupatikana
Aliongeza kuwa kulingana na jiografia ya eneo hilo ambalo lina vilima na mabonde linahitaji mnara zaidi ya mmoja ili kupatikana kwa huduma bora za mawasiliano ambapo kwa hatua za awali ni vizuri kuboresha mnara uliopo ili angalau wananchi waweze kupata huduma za mawasiliano wakati taratibu za Serikali za kujenga minara katika maeneo hayo zikiendelea kwa awamu
Akizingumzia upande wa malalamiko ya kuwa na redio yao Mkuu wa TCRA Kanda ya Kaskazini Mhandisi Imelda Salum amesema kuwa TCRA imeshatenga masafa kwa ajili ya Wilaya ya Same na ndani ya mwezi wa saba masafa hayo yatatangazwa ili wawekezaji wajitokeze kwa ajili ya kuanzisha redio ambayo itafikisha mawasiliano ya redio katika wilaya ya Same
Aidha, wawakilishi wa makampuni ya simu walioambatana nae katika ziara hiyo wameahidi kushughulikia changamoto za mawasiliano katika eneo hilo ambalo linaonekana kuwa na mvuto kibiashara ikiwa ni pamoja na kupeleka huduma ya laini za simu na vocha kwa upande wa kampuni ya Halotel
Naye Mbunge wa Same Mashariki Mhe. Anne Kilango Malecela ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu amezungumza na wananchi wake na kuwaambia kuwa Serikali inajali na kushughulikia kero na malalamiko ya wananchi wake kwa kuboresha upatikanaji wa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na huduma ya mawasiliano





Post a Comment